Mauritius yamwambia Trump: ‘Hakuna Mjadala’ kuhusu Chagos
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135772-mauritius_yamwambia_trump_hakuna_mjadala’_kuhusu_chagos
Umiliki wa Mauritius juu ya Visiwa vya Chagos hauna utata wowote na “haupaswi tena kuwa mada ya mjadala,” amesema Mwanasheria Mkuu wa taifa hilo la pwani ya Afrika Mashariki. Gavin Glover alitoa kauli hiyo akijibu matamshi ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuhusu uamuzi wa Uingereza kukabidhi tena udhibiti wa eneo hilo la Bahari ya Hindi kwa koloni lake la zamani.
(last modified 2026-01-22T16:48:56+00:00 )
Jan 22, 2026 10:31 UTC
  • Mauritius yamwambia Trump: ‘Hakuna Mjadala’ kuhusu Chagos

Umiliki wa Mauritius juu ya Visiwa vya Chagos hauna utata wowote na “haupaswi tena kuwa mada ya mjadala,” amesema Mwanasheria Mkuu wa taifa hilo la pwani ya Afrika Mashariki. Gavin Glover alitoa kauli hiyo akijibu matamshi ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuhusu uamuzi wa Uingereza kukabidhi tena udhibiti wa eneo hilo la Bahari ya Hindi kwa koloni lake la zamani.

Trump, kupitia chapisho lake katika ukurasa wa Truth Social siku ya Jumanne, amekosoa makubaliano ya Uingereza na Mauritius akiyataja kuwa kitendo cha “upumbavu mkubwa” na “udhaifu wa hali ya juu,” akidai kwamba Uingereza imeachana na “ardhi muhimu sana” inayohifadhi “kituo muhimu cha kijeshi cha Marekani.” Visiwa vya Chagos, vilitenganishwa na Mauritius na Uingereza mwaka 1965, miaka mitatu kabla ya taifa hilo la Afrika Mashariki kupata uhuru. Mwaka 1966, kisiwa kikubwa zaidi cha Chagos, Diego Garcia, kilipangishwa kwa Marekani kwa matumizi ya kijeshi, na takribani wakazi 2,000 walifurushwa. Tangu wakati huo, Mauritius imekuwa ikitaka kurejesha mamlaka yake juu ya eneo hilo.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, alitia saini makubaliano ya kuhamisha mamlaka ya visiwa hivyo kwa Mauritius mwezi Mei 2025. Hata hivyo, makubaliano hayo yanairuhusu Washington na London kuendelea kudhibiti kituo cha pamoja cha kijeshi kilichopo Diego Garcia kwa kipindi cha awali cha miaka 99, kwa thamani inayoripotiwa kufikia dola bilioni 3.9.

Waziri Mkuu wa Mauritius, Navin Ramgoolam, alisifu makubaliano hayo kama hatua ya kihistoria kuelekea “kukamilisha mchakato mzima wa ukoloni,” huku Starmer akisema wakati huo kwamba Trump aliunga mkono hatua hiyo. Katika taarifa yake, Mwanasheria Mkuu wa Mauritius, Gavin Glover, alisema makubaliano hayo “yalijadiliwa, kukamilishwa na kutiwa saini kikamilifu” kati ya Uingereza na Mauritius pekee. Aliongeza kuwa licha ya matamshi ya Trump, Mauritius “inasubiri utekelezaji wa mkataba huo haraka iwezekanavyo, kwa mujibu wa ahadi zilizotolewa."