Wanajeshi 8 wa Nigeria wauawa katika shambulio la Boko Haram Borno
Wanajeshi wanane wa Nigeria wameuawa huku wengine 50 wakijeruhiwa baada ya wapiganaji wa genge la kigaidi la Boko Haram kushambulia kambi ya kijeshi katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa nchi.
Vyanzo vya kiusalama vimeripoti hayo na kuongeza kuwa, wanamgambo hao walifika kwa pikipiki na magari ya deraya katika eneo la tukio.
Duru za kiusalama zimesema kikosi hicho cha kijeshi kilikuwa sehemu ya mashambulizi ya kuwaondoa waasi kutoka 'Timbuktu Triangle', ngome ya muda mrefu ya wanamgambo huko kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Jeshi la Nigeria lilisema jana Jumatano kuwa, askari wake walishambulia gari moja lililokuwa na mada za miripuko, lakini la pili liliweza kupenya safu za ulinzi, na kuwaua wanajeshi kadhaa na wanachama wa Kikosi Kazi cha Pamoja cha Raia, wapiganaji wa kiraia wanaoliunga mkono jeshi.
Wakati huo huo, jeshi la Nigeria limeripoti kuwa wanajeshi watano na afisa mmoja wa polisi wameuawa katika shambulizi la kuvizia kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
Jeshi la Nigeria jana lilitangaza habari ya kuwakomboa mateka 62 katika operesheni tofauti katika jimbo hilo la Zamfara, la kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
Haya yanajiri siku chache baada ya Jeshi la Anga la Nigeria kutangaza kuwa limeuwa takriban magaidi 40 wa Boko Haram katika mashambulizi ya anga mtawalia liliyoyafanya mapema wiki hii katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria.