Putin: Denmark imekuwa ikiitazama Greenland kama koloni lake
Rais wa Russia, Vladimir Putin amesema, Denmark imekuwa ikiichukulia Greenland kama koloni lake. Amesema hayo akitoa mtazamo wake kuhusu mpango wa Rais wa Marekani, Donald Trump wa 'kukinunua' kisiwa hicho cha Aktiki kinachojitawala.
"Daima Denmark imekuwa ikiitazama Greenland kama koloni, na kuamiliana nayo kwa ukali sana, kama si kwa ukatili," Putin amesema hayo akihutubia mkutano na Baraza la Usalama w Taifa la Russia katika Ikulu ya Kremlin jana Jumatano.
Putin amesema Russia haina ushiriki wowote katika mzozo kuhusu umiliki wa kisiwa hicho. "Hakika haituhusu. Nadhani watalitatua kati yao wenyewe," amesisitiza Rais wa Russia.
Trump ametangaza wazi kwamba, Marekani inataka kuimiliki Greenland kwa sababu za kiusalama, kiuchumi na kistratijia, na analitambua suala hili kuwa sehemu ya maslahi muhimu ya Marekani katika karne ya 21.
Hii ni katika hali ambayo, wakazi wa Greenland wamesisitiza kuwa kisiwa hicho ni mali ya kuuzwa. Kadhalika, maelfu ya wananchi wa Denmark walikusanyika katika mji wa Copenhagen hivi karibuni na kulaani madai na vitisho vya Trump vya kuikalia kwa mabavu Greenland.
Viongozi wa Ulaya pia wamechukua msimamo dhidi ya matakwa haya ya Trump. Katika radiamali zao kwa jaribio la Trump la kutwaa Greenland, nchi za Ulaya zimesisitiza kuwa, zitatetea mamlaka ya Denmark juu ya kisiwa hicho.