Lavrov: Ufaransa na Ukraine zinasaidia makundi ya kigaidi barani Afrika
-
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov, amesema kuwa Ufaransa na Ukraine zinatoa msaada kwa makundi ya kigaidi na mitandao ya waasi barani Afrika, ikiwemo matawi ya magaidi ISIS au Daesh.
Lavrov ametoa kauli hiyo alipokuwa akijibu swali kuhusu kile alichokiita kuingilia kwa nchi za Magharibi katika eneo la Sahel barani Afrika, wakati wa mkutano wa wanahabari uliolenga kutoa muhtasari wa shughuli za kidiplomasia za Russia kwa mwaka 2025.
Aidha ameikosoa Ufaransa kwa kile alichokitaja kama jaribio la “kila namna,” ikiwemo kutumia “mbinu za kigaidi,” ili kuzuia kuundwa kwa serikali thabiti katika makoloni yake ya zamani eneo la Sahel. Lavrov amesema kuna “ushahidi wa wazi” unaoonyesha kuwa shughuli kama hizo zinafanyika, zikiwemo zile zinazohusisha “mamluki wa Kiukraine… kwa lengo la kuidhuru Shirikisho la Russia na marafiki wetu popote duniani.”
Burkina Faso, Mali na Niger, ambao ni waanzilishi wa Muungano wa Nchi za Sahel (AES), wamekumbwa na mashambulizi mabaya ya kigaidi kwa zaidi ya muongo mmoja, yakichochewa na waasi na magaidi. Viongozi wa kijeshi wa nchi hizo walioingia madarakani kwa uungaji mkono wa wananchi wameendelea kuishutumu Paris na Kiev kwa kuunga mkono magaidi.
Nchi hizo tatu ambazo zamani zilikuwa makoloni ya Ufaransa zilijiondoa rasmi kutoka Muungano wa Kiuchumi wa Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, mwaka jana baada ya mapinduzi ya kijeshi kuyumbisha uhusiano wao na jumuiya hiyo. Ziliishutumu jumuiya ya kikanda kwa kushindwa kuwasaidia kupambana na ugaidi na kwa kutishia mamlaka yao ya kitaifa kwa kutumika kama chombo cha nmadola ya kigeni, hususan Ufaransa.
Russia, ambayo imefanya vita dhidi ya ugaidi kuwa nguzo kuu ya ushirikiano wake wa kiusalama na mataifa ya Afrika, imekuwa ikilaani mara kwa mara kuingilia kwa mataifa ya kigeni katika eneo la Sahel, ikiwemo kile inachokitaja kama “muungano wa kihalifu” wa Ufaransa na Ukraine na makundi yenye misimamo mikali katika eneo hilo.