Oct 06, 2024 07:28 UTC
  • Hizbullah yashambulia kampuni ya viwanda vya kijeshi vya Israel

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imeshambulia kwa mabomu kampuni ya viwanda vya kijeshi vya utawala wa Kizayuni ya "ETA".

Idara ya Habari ya Hizbullah ya Lebanon imetangaza kuwa: Ili kulitetea taifa thabiti la Palestina huko Gaza na kwa ajili ya kuilinda Lebanon na watu wake, na pia kukabiliana na mashambulizi ya kinyama ya Israel dhidi ya miji, vijiji na raia, wapiganaji wa Muqawama wa Kiislamu wameshambulia kwa makombora kadhaa kampuni ya zana kijeshi ya ETA inayomilikiwa na utawala wa Kizayuni katika maeneo ya Sukhnin na kambi ya Ma'ale Golani.

Wakati huo huo, vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vimekiri kwamba tangu asubuhi ya leo zaidi ya makombora 110 yamerushwa kutoka Lebanon kuelekea katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina.

Vyombo hivyo vya habari vimetangaza kuwa ving'ora vya tahadhari vimesikika katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni vya "Al-Mutla" na "Miskaf Aam" na kwamba sauti ya milipuko kadhaa imesikika katika maeneo hayo.

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imekuwa ikitekeleza operesheni nzito kila siku dhidi ya malengo na vituo vya kijeshi za Israel tangu utawala huo katili ulipoanzisha mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina wa Ukanda wa Gaza yapata mwaka mmoja uliopita.  

Tags