Israel yashambulia hospitali ya watoto Tehran na kuua shahidi kadhaa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i127620
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei ameulaani vikali utawala haramu wa Israel kwa kuwaua shahidi watoto katika vita vyake vya kichokozi vinavyoendelea dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
(last modified 2025-06-16T11:20:20+00:00 )
Jun 16, 2025 11:20 UTC
  • Israel yashambulia hospitali ya watoto Tehran na kuua shahidi kadhaa

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei ameulaani vikali utawala haramu wa Israel kwa kuwaua shahidi watoto katika vita vyake vya kichokozi vinavyoendelea dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Baqaei amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye akaunti yake ya X na kueleza kuwa, "Utawala wa Israel umeua watoto wengi katika kipindi cha siku 3 zilizopita za vita vyake vya kichokozi dhidi ya Iran na pia umelenga hospitali ya watoto (Hospitali ya Watoto ya Hakim inayohusishwa na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba cha Tehran)."

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amebainisha kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel "unaua watoto kama burudani" kama alivyowahi kukiri Yair Golan, naibu mkuu wa zamani wa jeshi la Israel.

Amesema "Katika mashambulizi matatu ya hivi karibuni yaliyotekelezwa na Israel jijini  Tehran, wanawake na watoto 73 wameuawa." Baghaei ameongeza kuwa "Watoto 20 waliouawa katika mtaa wa Chamran, 10 bado wamekwama chini ya vifusi."

Wakati huo huo, Saeed Khatibzadeh, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya utafiti, ameilaani Israel kwa kufanya uhalifu wa kivita kwa kulenga miundombinu ya wizara hiyo katika shambulio lake la anga dhidi ya Tehran.

Utawala mtenda jinai wa Israel usivyowasaza hata watoto wadogo

"Utawala wa kihalifu wa Israel umefanya hujuma za kimakusudi na za kikatili kwenye moja ya majengo ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, liliyoko mkabala na Taasisi ya Mafunzo ya Kisiasa na Kimataifa (IPIS)," Khatibzadeh ameandika kwenye mtandao wa X.

"Raia kadhaa walijeruhiwa katika shambulio hilo, ikiwa ni pamoja na idadi kubwa ya wafanyakazi wenzangu, ambao walipelekwa hospitalini kwa matibabu," amesema hayo na kuongeza kuwa, maktaba ya IPIS ililengwa katika "shambulio hili la woga" pia.

"Huu ni uhalifu mwingine wa wazi wa kivita, sehemu ya kampeni ya Israel inayoendelea na ya kimfumo ya uchokozi dhidi ya Iran," Khatibzadeh, ambaye pia ni mwenyekiti wa IPIS, aliongeza katika ujumbe wake huo katika mtandao wa kijamii wa X.