Iran yamyonga jasusi wa Mossad; msako dhidi ya maajenti wengine unaendelea
Iran mapema leo imetekeleza hukumu ya kumnyonga Esmail Fekri, jasusi aliyepatikana na hatia ya kushirikiana na shirika la kijasusi la Israel la Mossad.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mahakama ya Iran, wakati wa kukamatwa kwake, Fekri alikuwa akiwasiliana kikamilifu na watendaji wa Mossad.
Kwa mujibu wa kituo cha habari cha Idara ya Mahakama, Fekri amenyongwa Jumatatu asubuhi kufuatia mchakato kamili wa kisheria, ikiwa ni pamoja na kesi, rufaa, na uthibitisho wa mwisho wa hukumu na Mahakama ya Juu ya Iran.
Rekodi za mahakama zinaonyesha kwamba Fekri, alikuwa amedumisha mawasiliano na maafisa wawili wa Mossad na alijaribu kukusanya na kusambaza taarifa nyeti na zilizoainishwa za usalama wa taifa—kama vile maeneo ya kimkakati, maelezo ya watu mahususi, na misheni ya ndani ya shirika—kupitia njia salama za mawasiliano.
Jasusi huyo wa utawala wa Kizayuni wa Israel alikamatwa Desemba mwaka 2023 na vyombo vya usalama vya Iran alipokuwa akiwasiliana kikamilifu na maafisa wa Mossad.
Huku hayo yakijiri, vikosi vya usalama vya Iran vimewakamata magaidi wawili wa shirika hilo la ujasusi la utawala haramu wa Israel kaskazini magharibi mwa Iran. Kamandi Polisi ya Iran imetangaza kuwa, maajenti hao wawili wa Mossad walikamatwa katika Kaunti ya Savojbolagh mkoani Alborz, kaskazini magharibi mwa Iran.
Taarifa hiyo imesema: "Kupitia juhudi za polisi wa mkoa wa Alborz, wanachama wawili wa kundi la kigaidi linalofungamana na Mossad walikamatwa." Taarifa hiyo imebaini kuwa, magaidi hao walikuwa wakitengeneza mabomu, vilipuzi, mitego , na vifaa vya kielektroniki katika nyumba moja ya kundi hilo. Shirika la kijasusi na kigaidi la Mossad husimamia na kufadhili shughuli za kijasusi na operesheni za siri nje ya mipaka ya utawala haramu wa Israel.