Malaki waandamana Hague, Brussels kuonyesha mshikamano na Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i127618
Makumi ya maelfu ya watu waliovalia mavazi mekundu wameandamana katika mitaa ya mji wa Hague nchini Uholanzi na mjini Brussels huko Ubelgiji kuonyesha mshikamano na Wapalestina wa Gaza sanjari na kushinikiza hatua zaidi kutoka kwa serikali zao dhidi ya mauaji ya kimbari katika eneo hilo la Palestina lililozingirwa.
(last modified 2025-07-16T03:27:25+00:00 )
Jun 16, 2025 10:22 UTC
  • Malaki waandamana Hague, Brussels kuonyesha mshikamano na Gaza

Makumi ya maelfu ya watu waliovalia mavazi mekundu wameandamana katika mitaa ya mji wa Hague nchini Uholanzi na mjini Brussels huko Ubelgiji kuonyesha mshikamano na Wapalestina wa Gaza sanjari na kushinikiza hatua zaidi kutoka kwa serikali zao dhidi ya mauaji ya kimbari katika eneo hilo la Palestina lililozingirwa.

Huko mjini Brussels nchini Ubelgiji, makumi ya maelfu ya watu wlaioshiriki maandamano hayo ya jana Jumapili wameutaka Umoja wa Ulaya kuchukua hatua za kukomesha mauaji hayo ya halaiki Gaza. Waliojitokeza kwenye maandamano hayo walikadiriwa kuwa 110,000 na waandaaji.

Makundi ya kutetea haki za binadamu kama vile Amnesty International na Oxfam yaliandaa maandamano hayo, ambayo yalilenga kuunda vuguvugu la "mstari mwekundu" la kutaka kukomeshwa mauaji ya kimbari Gaza.

Wakati huo huo, mji wa Hague ulishuhudia maandamano mengine ya kuitetea Palestina jana, ambapo baadhi ya waandamanaji walipeperusha bendera za Palestina huku wengine wakipiga nara za "Komesha Mauaji ya Kimbari". Waandamanaji katika mji huo wa Uholanzi waligeuza bustani ya katikati ya mji kuwa bahari ya rangi nyekundu kabla ya maandamano hayo kuelekea nje ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ.

Watu zaidi ya 150,000 walishiriki katika maandamano hayo huko Hague nchini Uholanzi kwa mujibu wa waandaaji wa maandamano hayo ya kutangaza mshikamano na Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

 "Zaidi ya watu 150,000 hapa wamevaa nguo nyekundu, na idadi kubwa ya Waholanzi - wanataka tu vikwazo madhubuti (dhidi ya Israel) ili kukomesha mauaji ya kimbari huko Gaza," amesema Michiel Servaes, Mkurugenzi wa Oxfam Novib, tawi la Uholanzi la shirika hilo la kimataifa la misaada.

Huko Ufaransa siku ya Jumamosi, maelfu ya watu wengine walijiunga na maandamano kama hayo, kama sehemu ya uhamasishaji wa wikendi kote ulimwenguni dhidi ya uvamizi wa Israeli katika ardhi ya Palestina.

Roma, mji mkuu wa Italia, Jumamosi iliyopita pia ulishuhudia mojawapo ya maandamano makubwa zaidi dhidi ya Israel barani Ulaya. Idadi kadhaa ya watu mashuhuri wa kisiasa na kijamii wa Italia walihutubia pambizoni mwa maandamano hayo ambapo huku wakiashiria wajibu wa kimaadili na kihistoria wa Ulaya, walitaka kusitishwa uuzaji wa silaha kwa Israel.