Je, kwa nini Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halikulaani Israel?
Kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichofanyika kwa ombi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kufuatia mashambulizi ya kijeshi ya utawala wa Israel dhidi ya Iran, kwa mara nyingine tena kimefichua siasa za kundumakuwili za kimataifa na mapungufu makubwa yaliyoko katika muundo wa Baraza la Usalama.
Katika kikao hicho kilichofanyika chini ya anwani "Vitisho kwa Amani na Usalama wa Kimataifa," baadhi ya wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama vile Russia na China walilaani uchokozi wa Tel Aviv dhidi ya Iran, baadhi wakieleza wasiwasi wao kuhusu kuongezeka mivutano katika Mashariki ya Kati na kutaka kuendelezwa diplomasia kwa ajili ya kutatua matatizo, huku Marekani na nchi za Ulaya zikiendelea kutetea sera za uchokozi wa Israel dhidi ya Iran.
Kikao hicho kimefanyika katika hali ambayo mashambulizi ya Israel dhidi ya shabaha kadhaa nchini Iran yamepelekea kuuawa kigaidi kwa makamanda kadhaa wa ngazi za juu jeshini, wanasayansi na raia wa kawaida. Israel pia imelenga vituo vingi vya nyuklia vya Iran kwa kisingizio cha hatari ya shughuli zake kuzalisha silaha za nyuklia.
Katika kikao hicho baadhi ya wanachama walilichukulia shambulio hilo kama ukiukaji wa wazi wa Hati ya Umoja wa Mataifa na wakataka jibu madhubuti litolewe na Baraza la Usalama huku wengine wakionyesha wasiwasi wao wa maneno matupu na hivyo kuepuka kuchukua msimamo wa wazi kuhusu suala hilo. Wengine kama vile Marekani, waliitetea Israel kwa nguvu zao zote wakidai kuwa hiyo ni hatua ya Tel Aviv kujilinda.
Katika matamshi yake katika kikao hicho, Vassily Nebenzia Mwakilishi wa kudumu wa Russia katika Umoja wa Mataifa alisema kwamba mashambulizi ya Israel katika ardhi ya Iran hayakuchochewa na chochote kile bali ni ya kichokozi na yasiyohalalishwa kwa njia yoyote ile. Alisema, "Jamii ya kimataifa haiwezi na wala haipaswi kukaa kimya kuhusu uchokozi huo wa wazi." Fu Kong, Mwakilishi wa China pia alichukua msimamo sawa na huo na kusema kwamba kuongezeka kwa mivutano katika eneo hilo hakutamnufaisha yeyote, na kusisitiza kwamba kuharibiwa vituo vya nyuklia vya Iran kufuatia mashambulizi hayo kunaweza kuwa na madhara makubwa ya kimazingira na kibinadamu, na kwamba tabia hiyo inakiuka kanuni za kimsingi za sheria za kimataifa.

Israel imelenga maeneo ya nyuklia ya Iran na kuwaua wanasayansi wake wa nyuklia, hatua ambayo ni kinyume cha sheria zote za kimataifa. Pamoaj na hayo, nchi za Magharibi na Marekani zimefumbia macho ukweli huo na kuamua kukaa kimya. Kuhusu hilo, tunaweza kutaja misimamo ya kuchekesha ya nchi kama vile Ufaransa na Ujerumani ambazo zilitafsiri hatua hiyo ya Israeli kama ya kujilinda na hivyo kutoilaani. Baadhi ya nchi pia zilichukua misimamo yenye utata na isiyo na maamuzi ya wazi, zikiwemo Ugiriki, Denmark, Korea Kusini na Panama, ambazo zote zilionyesha wasiwasi wao wa kidhahiri tu kuhusu kuongezeka kwa mivutano katika eneo, lakini zikakataa kuingia kwenye mjadala kuhusu uhalali au uharamu wa shambulio hilo.
Katika kukabiliana na mijadala hii tofauti, kinachotia wasiwasi zaidi ni kimya kizito cha Umoja wa Mataifa na taasisi zake zinazohusika na hatua za moja kwa moja za kijeshi dhidi ya mmoja wa wanachama wake. Ijapokuwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA umetoa ripoti kuhusu hali ya vituo vya Iran, lakini haukuchukua msimamo wowote wa kisheria au kiufundi kuhusu tishio linalohatarisha usalama wa vituo vya vya nyuklia vya Iran ambako shughuli za kiraia za nyuklia zinaendelea. Bila shaka huo ni undumakuwili wa wazi katika mpangilio wa kimataifa, suala ambalo hufanya maamuzi muhimu ya kimataifa kuchukuliwa kwa mitazamo ya kisiasa na miungano ya nguvu, na sio kwa kuzingatia sheria na Hati ya Umoja wa Mataifa.
Bila shaka, hatua ya kijeshi ya Israel dhidi ya ardhi ya Iran hususan ya kulenga miundombinu ya kiraia na vituo vya amani vya nyuklia, si tu kwamba ni ukiukaji wa wazi wa Hati ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa, bali pia ni ukiukaji mkubwa wa mikataba ya kimataifa kuhusu usalama wa nyuklia. Kwa kuzingatia kanuni zinazotambulika za kimataifa, hususan Azimio 487 la Baraza la Usalama (lililopitishwa mwaka 1981), ambalo lililaani shambulio kama hilo la Israel dhidi ya kinu cha nyuklia cha Iraq, jamii ya kimataifa inawajibika kujibu shambulio lolote dhidi ya vituo vya nyuklia vya nchi yoyote ile. Hasa wakati vifaa hivi vinafanya kazi chini ya usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na ndani ya mfumo wa NPT. Pamoja na hayo la kusikitisha ni kwamba Baraza la Usalama sio tu kwamba limeshindwa kujibu ipasavyo shambulio hilo la kichokozi, bali pia limeamu kunyamazia kimya hatua hiyo hatari ya Israel.
Kwa hakika, kimya cha taasisi za kimataifa, ikiwa ni pamoja na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA, kuhusu suala hili kinatia wasiwasi mkubwa na bila shaka ni jambo lisilokubalika kabisa. Chombo hiki mahimu, ambacho kina jukumu la kusimamia shughuli za amani za nyuklia, hakijawa tayari kuchukua msimamo wa kisheria wa kukabiliana na shambulio la moja kwa moja kwenye vituo vilivyo chini ya usimamizi wake. Tabia hii sio tu inapunguza imani kwa wakala huo miongoni mwa nchi wanachama, bali pia inauweka kwenye utegemezi wa kisiasa, suala ambalo linatilia shaka kubwa utendakazi wake wa kiufundi unaopasa kutopendelea upande wowote katika shughuli zake za kiufundi.
Ni wazi kwamba ili Umoja wa Mataifa na taasisi zake zijizuie kuwa chombo cha kutumikia madola yenye nguvu, ni lazima zivunje kimya chao mbele ya uchokozi wa wazi wa Israel dhidi ya mataifa mengine na kuzingatia sheria iliyojengeka kwenye misingi ya haki, usawa kwa mataifa yote na amani ya kudumu.