Kwa nini Marekani imeitaka China iache kununua mafuta ya Iran?
Waziri wa Fedha wa Marekani ametoa wito kwa China kuacha kununua mafuta ya Iran na Russia wakati huu inapokaribia duru mpya ya mazungumzo ya ushuru wa forodha kati ya Marekani na China.
Scott Bessent ametangaza kuwa kusitisha ununuzi wa mafuta kutoka Iran na Russia itakuwa moja ya mada kuu ya majadiliano katika mazungumzo ya wiki ijayo na maafisa wa China. Amesema, "Ikiwa China itaacha kununua mafuta kutoka Russia na Iran kwa muda wa miezi mitatu hadi sita, mashine ya vita ya Russia itazimwa na mazungumzo na Iran yatakuwa rahisi zaidi."
Matamshi hayo yametolewa kabla ya duru ya tatu ya mazungumzo ya kiuchumi kati ya Washington na Beijing, ambayo yamepangwa kufanyika mjini Stockholm leo Jumatatu na Jumanne ijayo. Bessent alisema uhusiano wa kibiashara kati ya Marekani na China sasa uko katika "hali nzuri," na kwamba hii imeruhusu masuala nyeti zaidi, ikiwa ni pamoja na mafuta na vikwazo, kushughulikiwa.
Hii ni katika hali ambayo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, amepinga madai yaliyotolewa na Waziri wa Fedha wa Marekani mnamo Julai 22 aliyesema kwamba "duru mpya ya mazungumzo kati ya nchi hizo mbili juu ya ushuru wa forodha inaweza pia kujumuisha ununuzi wa mafuta wa Beijing kutoka Tehran na Moscow" na kusisitiza kwamba msimamo wa nchi yake juu ya ushuru umekuwa wazi na thabiti siku zote.
China imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kwamba katika maamuzi yake ya kiuchumi, inafanya kazi kwa kuzingatia maslahi na kanuni za ushirikiano sawa, na inapinga mashinikizo au vikwazo vyovyote vya upande mmoja. Mwezi uliopita, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China alijibu matamshi ya Rais wa Marekani, Donald Trump akisema kwamba "China itachukua hatua zinazofaa kwa ajili ya kudhamini usalama wa nishati kwa kuzingatia maslahi yake ya kitaifa."
China na Iran zimekuwa na uhusiano mkubwa wa mafuta kwa miongo kadhaa, na uhusiano huo umekuwa iimara na wa kimkakati zaidi katika miaka ya hivi karibuni, licha ya vikwazo vya Marekani. Inafaa kukumbusha kuwa, Iran ilikuwa mmoja wa wauzaji wakuu wa mafuta kwa China kabla ya 2018, na kampuni za China zimeshiriki katika kustawisha maeneo ya mafuta ya Iran.
Kama sehemu ya kampeni ya mashinikizo ya juu zaidi ambayo ilitekelezwa wakati wa muhula wa kwanza wa rais Donald Trump (kuanzia Mei 2018, baada ya Marekani kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA), Marekani ilikuwa imejiwekea lengo la kupunguza mauzo ya mafuta ya Iran nje ya nchi hadi sifuri. Hata hivyo, kampeni hiyo ilishindwa kufikia lengo lililotajwa mwisho wa muhula wa kwanza wa Trump. Baada ya Trump kurejea White House mwishoni mwa Januari 2025, kwa mara nyingine tena alianzisha kampeni ya shinikizo la juu dhidi ya Iran kwa lengo lile lile la kupunguza mauzo ya mafuta ya Iran hadi sifuri. Ikizingatiwa kuwa China ndio mnunuzi mkuu wa mafuta ya Iran, utawala wa Trump unajaribu kutumia suala hili kama chombo katika mazungumzo ya ushuru na China ili kuishinikiza Beijing isitishe kununua mafuta ya Iran. Hata hivyo mbinu hii ya Washington, kama ilivyoelezwa katika taarifa ya msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, imekabiliwa na upinzani kutoka Beijing.
Jambo muhimu ni kwamba, mauzo ya mafuta ya Iran yalivunja rekodi mwezi Juni 2025, na kufikia mapipa milioni 1.8 kwa siku, jambo ambalo ni pigo kubwa kwa sera ya vikwazo ya utawala wa Trump dhidi ya Iran.
Juhudi za marais wa Marekani (hasa Donald Trump) za kuweka vikwazo vikali na vikubwa zaidi dhidi ya Iran (hasa katika sekta ya mafuta) zimekuwa na lengo la kudhibiti na kuilazimisha Iran ikubali matakwa haramu na yasiyo na mantiki ya Marekani (ikiwa ni pamoja na katika nyanja za teknolojia ya nyuklia, sera za kikanda na uwezo wa makombora wa Jamhuri ya Kiislamu). Hata hivyo Iran imeweza kuendelea kuuza mafuta nje ya nchi kwa kutumia mbinu mbalimbali, na China ikiwa mnunuzi mkuu wa mafuta ya Iran, imeendelea kununua bidhaa hiyo licha ya vitisho na shinikizo kutoka Marekani. Kwa hivyo, duru mpya ya mazungumzo ya kibiashara na Marekani huko Stockholm haitarajiwi kusalimu amri kwa matakwa ya Washington ya kuacha kununua mafuta kutoka Iran na Russia.
Jarida la Foreign Policy la Marekani limeandika katika makala yenye kichwa cha meneno: Vikwazo vya Mafuta Havifanyi Kazi Tena, kwamba: Enzi ya vikwazo vya mafuta kama chombo cha kulazimisha matakwa ya upande mmoja, imekwisha. Soko la mafuta la Iran limeundwa kwa mujibu wa hali mpya iliyotengenezwa na vikwazo. Katika hali zote mbili, vikwazo havijaweza kubadili mienendo ya serikali za nchi mbalimbali.