Sudan yaalaani tamko la RSF la kutangaza serikali nyingine nchini humo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128852
Serikali ya Sudan imelaani tangazo la Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) la kuundwa serikali sambamba na kulitaja kuwa ni "ushahidi wa kushindwa na kusambaratika kwa kundi hilo."
(last modified 2025-07-28T08:33:02+00:00 )
Jul 28, 2025 07:22 UTC
  • Sudan yaalaani tamko la RSF la kutangaza serikali nyingine nchini humo

Serikali ya Sudan imelaani tangazo la Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) la kuundwa serikali sambamba na kulitaja kuwa ni "ushahidi wa kushindwa na kusambaratika kwa kundi hilo."

Taarifa ya serikali ya Sudan imesema Khartoum inalaani tamko la Vikosi vya Msaada wa Haraka kuhusu serikali ghushi, ambayo inapuuza kabisa mateso ya watu wa Sudan, ambao imewasulubu kwa aina zote za unyanyasaji, ukatili na mateso.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kutolewa tangazo hilo kwenye mitandao ya kijamii ni "ushahidi bora zaidi wa kushindwa na kusambaratika kwa kundi la RSF kwa mikononi ya majeshi yetu mashujaa, pamoja na makundi na washirika wao."

Taarifa hiyo pia imelaani hatua ya Kenya ya kuwa mwenyeji wa mikutano ya maandalizi ya tangazo la serikali sambamba na kusisitiza kwamba hatua hiyo ni ukiukaji wa uhuru wa Sudan na inakinzana na kanuni na mikataba ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Mamlaka ya Maendeleo ya Kiserikali (IGAD) katika kuunga mkono umoja na mamlaka ya Sudan.

Sudan pia imetoa wito kwa nchi jirani, jamii ya kimataifa na mashirika ya kikanda na kimataifa kulaani na kutolitambua tamko hilo.

Kundi la Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) Jumamosi iliyopita lilitangaza kuundwa kwa serikali sambamba nchini Sudan, hatua ambayo Umoja wa Mataifa ulikuwa umeonya hapo awali kuwa itakuwa tishio kwa umoja wa ardhi ya Sudan.