Wasiwasi watanda, magaidi wakilenga tena kambi za polisi wa Kenya, Lamu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128848-wasiwasi_watanda_magaidi_wakilenga_tena_kambi_za_polisi_wa_kenya_lamu
Vikosi vya kulinda usalama msituni Boni, Kaunti ya Lamu nchini Kenya, vimezidisha msako dhidi ya magaidi wanaohusishwa na kundi la Al-Shabaab, baada ya jaribio jingine la kuvamia kambi ya polisi wa GSU.
(last modified 2025-07-28T03:50:56+00:00 )
Jul 28, 2025 03:50 UTC
  • Wasiwasi watanda, magaidi wakilenga tena kambi za polisi wa Kenya, Lamu

Vikosi vya kulinda usalama msituni Boni, Kaunti ya Lamu nchini Kenya, vimezidisha msako dhidi ya magaidi wanaohusishwa na kundi la Al-Shabaab, baada ya jaribio jingine la kuvamia kambi ya polisi wa GSU.

Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, magaidi hao wamejaribu kuvamia kambi za GSU kwenye vijiji tofauti vya msitu wa Boni lakini majaribio yao yamezimwa.

Jaribio la karibuni zaidi ni la Ijumaa iliyopita, ambapo magaidi wapatao 60 wa Al-Shabaab waliokuwa wamejizatiti kwa silaha hatari walijaribu kuingia katika kambi ya pilisi wa GSU Basuba kwa lengo la kuilipua lakini walikabiliwa na majibu makali na kuzidiwa nguvu.

Hujuma hiyo ilifanyika majira ya saa tatu unusu usiku, ambapo magaidi wa Al Shabab walijitokeza msituni na kuanza kufyatua risasi kila upande kuilenga kambi hiyo.

Vilevile walijaribu kurusha marokote ya RPG ili kuimaliza kambi hiyo lakini walizidiwa nguvu, hivyo kutokomea kwenye vichaka vya msitu wa Boni.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Wesley Koech, amesema: “Oparesheni kali inaendelea msituni Boni na doria za walinda usalama zimeongezwa." Vilevile amewataka wananchi washirikiane na vikosi vya usalama kwa kutoa taarifa zitakazosaidia "kumshinda adui".