DRC yaishtaki Rwanda ICJ kwa tuhuma za unyanyasaji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i139478-drc_yaishtaki_rwanda_icj_kwa_tuhuma_za_unyanyasaji
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imewasilisha kesi dhidi ya Rwanda katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ, ikiituhumu nchi hiyo jirani kwa vitendo vya ukatili katika eneo lenye utajiri wa madini la mashariki mwa DRC.
(last modified 2026-06-28T04:33:58+00:00 )
Jun 28, 2026 04:32 UTC
  • DRC yaishtaki Rwanda ICJ kwa tuhuma za unyanyasaji

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imewasilisha kesi dhidi ya Rwanda katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ, ikiituhumu nchi hiyo jirani kwa vitendo vya ukatili katika eneo lenye utajiri wa madini la mashariki mwa DRC.

Hali hiyo inachagizwa na uwepo wa makundi mengi yenye silaha ikiwa ni pamoja na kundi la M23, ambalo limeteka na kudhibiti maeneo makubwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na linalotuhumiwa na serikali ya Kinshasa kuwa linaungwa mkono na Rwanda, Madai ambayo yamekuwa yakikanushwa na serikali ya Kigali.

Mahakama ya ICJ imeeleza kuwa DRC inaishutumu Rwanda kwa makosa yaliyofanywa kama sehemu ya "kampeni ya kupinga mauaji ya halaiki na ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu" huko mashariki mwa DRC tangu mwaka 1996, na kwamba wanaolengwa ni jamii ya wahutu kutokana na mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994.

Serikali ya Kinshasa imeitaka mahakama hiyo kuiwajibisha Rwanda kwa madai ya ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa.

Waziri wa Sheria wa Congo DR, Guillaume Ngefa Atondoko Andali, amethibitisha hatua hiyo akisema Kinshasa imechukua mkondo wa kisheria kama sehemu ya dhamira yake ya kutatua migogoro kwa njia za amani chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Hadi sasa, mamlaka za Rwanda hazijatoa tamko kuhusu kesi hiyo. Hata hivyo, wachambuzi wa sheria za kimataifa wanasema kesi hiyo inaweza kukabiliwa na changamoto za kisheria kuhusu mamlaka ya mahakama kuisikiliza bila ridhaa ya Rwanda au msingi mwingine wa kisheria unaoifunga nchi hiyo.