Satelaiti ya Nahid-2 ya Iran yatulia anga za mbali, yatuma taarifa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i128862-satelaiti_ya_nahid_2_ya_iran_yatulia_anga_za_mbali_yatuma_taarifa
Mkurugenzi wa Shirika la Anga la Iran (ISA), Hossein Salariyeh, amethibitisha kupokewa kwa taarifa za awali za telemetry kutoka kwa satelaiti ya Nahid-2 iliyozinduliwa hivi karibuni, akisema ishara hizo zinaonesha kuwa kifaa hicho kiko salama na kinafanya kazi kama ilivyokusudiwa ndani ya obiti yake maalum.
(last modified 2025-07-28T09:37:13+00:00 )
Jul 28, 2025 09:37 UTC
  • Satelaiti ya Nahid-2 ya Iran yatulia anga za mbali, yatuma taarifa

Mkurugenzi wa Shirika la Anga la Iran (ISA), Hossein Salariyeh, amethibitisha kupokewa kwa taarifa za awali za telemetry kutoka kwa satelaiti ya Nahid-2 iliyozinduliwa hivi karibuni, akisema ishara hizo zinaonesha kuwa kifaa hicho kiko salama na kinafanya kazi kama ilivyokusudiwa ndani ya obiti yake maalum.

Akizungumza na Press TV Jumapili, siku mbili baada ya uzinduzi kutoka Vostochny Cosmodrome, kituo cha kurushia setilaiti kilichoko mashariki mwa Russia, Salariyeh amesema malengo ya sasa ni kufanya majaribio ya kina kwa kila sehemu ya mfumo wa setilaiti hiyo ili kuhakikisha inafanya kazi ipasavyo.

Alifafanua zaidi kuwa Nahid-2 ni setilaiti ya mawasiliano inayotumia teknolojia ya Ku-band, inayotumika sana katika mawasiliano ya kasi ya juu duniani kote. Kiongozi huyo wa Shirika la Anga la Iran alisisitiza kuwa shirika lake limefanya uchunguzi na tathmini ya kina kuhusu ubora wa muundo na vifaa vya setilaiti hiyo.

Amesema: “Hii ikiwa satelaiti ya kwanza ya Iran kufika obitini, tunalenga hasa kuchunguza muundo wake wa ndani na vifaa vyake. Kwa utaratibu wetu wa kawaida, hatua ya awali ni kuistahimilisha katika obiti na kudhibiti vipengele vinavyohusiana na hali ya kifaa hicho."

Salariyeh ameongeza kuwa uzinduzi uliofanikiwa wa Nahid-2 ni hatua kubwa katika maendeleo ya uwezo wa anga wa taifa, na amebainisha kuwa ujenzi wa kizazi kijacho cha Nahid-3 tayari unaendelea.

Setilaiti ya Nahid-2, iliyotengenezwa nchini Iran, ilirushwa kwa mafanikio katika obiti ya kilomita 500 Ijumaa, Julai 25, kwa kutumia roketi ya Kirusi aina ya Soyuz.

Imeundwa kutoa uwezo mpana wa mawasiliano na utafiti, Nahid-2 itawezesha usafirishaji salama wa data, kuhifadhi taarifa ndani ya chombo chenyewe, na kuunganisha moja kwa moja na kituo cha udhibiti wa misheni.

Wachambuzi wa masuala ya anga wameitaja kama mafanikio makubwa katika miundombinu ya Iran ya mawasiliano ya angani. Kwa mara ya kwanza katika mfululizo wa satelaiti za Jamhuri ya Kiislamu, Nahid-2 pia itatumiwa kama jukwaa la majaribio ya mifumo ya kuendesha kwa gesi ya kemikali na gesi moto, teknolojia zinazotumika kudhibiti mwelekeo sahihi wa setilaiti katika obiti.

Kwa kuongeza ubunifu wake, satelaiti hiyo itafanya ufuatiliaji wa nafasi bila kutumia GPS, bali itatumia data ya Two-Line Element (TLE), mfumo sanifu wa kibunifu unaowezesha kufuatilia nafasi ya satelaiti kwa njia ya kujitegemea angani.