Uholanzi yatangaza Israel kuwa tishio la usalama
https://parstoday.ir/sw/news/world-i128870-uholanzi_yatangaza_israel_kuwa_tishio_la_usalama
Uholanzi, kupitia Ofisi ya Kuratibu Usalama na Kukabiliana na Ugaidi (NCTV), imetangaza kwa mara ya kwanza kuwa utawala wa Israel ni tishio la usalama kitaifa, kutokana na kampeni zake za upotoshaji wa taarifa na vitisho dhidi ya taasisi za kimataifa za haki.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Jul 28, 2025 09:42 UTC
  • Uholanzi yatangaza Israel kuwa tishio la usalama

Uholanzi, kupitia Ofisi ya Kuratibu Usalama na Kukabiliana na Ugaidi (NCTV), imetangaza kwa mara ya kwanza kuwa utawala wa Israel ni tishio la usalama kitaifa, kutokana na kampeni zake za upotoshaji wa taarifa na vitisho dhidi ya taasisi za kimataifa za haki.

Ripoti iitwayo Tathmini ya Vitisho kutoka kwa Mataifa iliyotolewa Julai 17, 2025, imeeleza kuwa Israel imekuwa ikijaribu mara kwa mara kushawishi maoni ya wananchi wa Uholanzi na kuathiri maamuzi ya kisiasa kupitia kampeni za taarifa potofu.

Ripoti hiyo imeeleza tukio la wizara ya Israeli kutumia njia zisizo rasmi kueneza hati yenye maelezo ya binafsi yasiyo ya kawaida kuhusu raia wa Uholanzi, ikiwalenga waandishi wa habari na wanasiasa.

Tukio hilo lilitokea baada ya mashabiki wa timu ya soka ya Maccabi Tel Aviv kuibua ghasia na fujo baada ya kushindwa kwa timu hiyo katika mechi ya Amsterdam mnamo Novemba 2024, jambo lililosababisha mvutano na ghasia na wenyeji wa jiji hilo.

Ripoti hiyo pia imeonyesha wasiwasi kuhusu vitisho dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) mjini The Hague, vilivyotolewa na Israel pamoja na Marekani, ikiainisha kuwa vitisho hivyo vinaweza kudhoofisha kazi ya mahakama hiyo.

Taarifa hiyo imesema Uholanzi ina "wajibu maalum" kulinda taasisi za kimataifa za sheria zinazopatikana katika ardhi yake.

Haya yanajiri sambamba na uchunguzi wa The Guardian Mei 2024 uliobainisha kuwa Israel imekuwa ikitishia ICC kwa muda mrefu, ikiwemo kampeni ya uonevu na vitisho dhidi ya maafisa wake, ili kuzuia uchunguzi wa madai ya uhalifu wa kivita.

Kwa mujibu wa wataalam wa sheria, juhudi za mashirika ya kijasusi ya Israel kuvuruga na kushawishi ICC zinaweza kuchukuliwa kama "makosa dhidi ya utawala wa sheria" na zinastahili kuchunguzwa na mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama hiyo.

Marekani, mshirika mkuu wa Israel, pia imeweka vikwazo dhidi ya ICC kufuatia kutolewa kwa hati za kukamatwa kwa waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na aliyekuwa waziri Yoav Gallant mwaka jana.

Mahakama ya ICC imekemea vikwazo hivyo, ikivitaja kuwa "jaribio la wazi" la kudhoofisha uhuru wake wa kimahakama.

Israel na Marekani si wanachama wa Mkataba wa Roma wa mwaka 1998 uliounda ICC, wala si washiriki wa mahakama hiyo.

Kupitia vikwazo hivyo, majaji wanne wanawake wa ICC wamezuiwa kuingia Marekani, huku mali au maslahi yao katika taifa hilo yakifungiwa.