UN yasema SDG hatarini kuweza kufikiwa katika anga ya kisiasa iliyopo
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametoa wito kwa dunia kuongeza kasi na dhamira ya kweli katika kutekeleza Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yanayofikia ukomo wake 2030, akisisitiza kuwa malengo hayo yako hatarini kuweza kufikiwa katika anga ya kisiasa iliyopo hivi sasa duniani.
Guterres ameyasema hayo alipohutubia mawaziri wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wakati wa Kongamano la Kisiasa la Ngazi ya Juu la 2025 kuhusu Maendeleo Endelevu lililofanyika mjini New York.
Kongamano hilo ni jukwaa la Umoja wa Mataifa la kukagua Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu.
"Malengo ya Maendeleo Endelevu sio ndoto. Ni mpango. Mpango wa kutimiza ahadi zetu kwa watu walio hatarini zaidi, kwa kila mmoja, na kwa vizazi vijavyo," ameeleza Katibu Mkuu wa UN.
Kulingana na ripoti ya hivi majuzi ya Umoja wa Mataifa, ni asilimia 35 pekee ya malengo ya maendeleo endelevu ndio yanakaribia kufikia malengo yao ifikapo mwaka 2030.
Guterres amesema, vita na hatari za dunia zinayasukuma mbali malengo ya SDGs na kuyafanya yawe hatarini kuweza kufikiwa.
"Uchumi wa kimataifa unapungua. Mivutano ya kibiashara inaongezeka. Kutokuwepo kwa usawa kunaongezeka. Bajeti za misaada zinapunguzwa huku matumizi ya kijeshi yakiongezeka. Na kutoaminiana, mgawanyiko na migogoro ya moja kwa moja vinauweka mfumo wa kimataifa wa kutatua matatizo kwenye utatizaji ambao haujawahi kushuhudiwa," amebainisha Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Viongozi wa dunia walipitisha ajenda mwaka 2015, ikiwa ni ramani ya njia ya kumaliza umaskini, kulinda sayari na kukabiliana na ukosefu wa usawa…/