Viongozi wa dunia wafika Tehran kutoa heshima kwa Kiongozi Shahidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i139624-viongozi_wa_dunia_wafika_tehran_kutoa_heshima_kwa_kiongozi_shahidi
Viongozi waandamizi wa Iran, marais na wakuu wa nchi, pamoja na wageni mashuhuri na wajumbe wa ngazi za juu kutoka mataifa mbalimbali duniani, wamefika Tehran kutoa heshima zao kwa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei.
(last modified 2026-07-04T05:19:36+00:00 )
Jul 04, 2026 04:28 UTC
  • Viongozi wa dunia wafika Tehran kutoa heshima  kwa Kiongozi Shahidi

Viongozi waandamizi wa Iran, marais na wakuu wa nchi, pamoja na wageni mashuhuri na wajumbe wa ngazi za juu kutoka mataifa mbalimbali duniani, wamefika Tehran kutoa heshima zao kwa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei.

Katika hafla iliyojaa uzito wa kihistoria na maombolezo, iliyofanyika Ijumaa katika Ukumbi wa Sala wa Tehran (Mosalla), wakuu wa mihimili mitatu ya utawala Iran, serikali kuu, bunge na mahakama, wakiongozana na marais, maspika wa mabunge, wajumbe maalum, wanazuoni, wasomi wa dini na wanafikra kutoka pembe mbalimbali za dunia, walihudhuria hafla ya kutoa heshima kwa Shahidi Ayatullah Khamenei.

Miongoni mwa waliohudhuria walikuwa Rais wa Iran Masoud Pezeshkian, Spika wa Bunge Mohammad Baqer Qalibaf, Mkuu wa Mahakama Gholam-Hossein Mohseni Eje’i, na Mwenyekiti wa Baraza la Kuainisha  Maslahi ya Mfumo Ayatullah Sadeq Amoli Larijani.

Ujio wa viongozi na wajumbe kutoka mataifa tofauti ulikuwa ishara ya uzito wa urithi wa Ayatullah Khamenei, si tu ndani ya Iran na ulimwengu wa Kiislamu, bali pia miongoni mwa watetezi wa uhuru na haki duniani.

Miongoni mwa viongozi waliofika ni pamoja na  mwenyekiti wa Baraza la Watu la Turkmenistan Gurbanguly Berdimuhamedow, Rais wa Iraq Nizar Amedi; Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan; Rais wa Tajikistan Emomali Rahmon; Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif pamoja na Mkuu wa Jeshi, Jenerali Asim Munir; na Rais wa Serikali ya eneo linalojitawala la Kurdistan nchini Iraq Nechirvan Barzani.

Pia maspika wa mabunge ya Iraq, Azerbaijan, Bangladesh, Uzbekistan, Belarus na Kyrgyzstan; mawaziri wa mambo ya nje wa Nicaragua, Jamhuri ya Congo na Burkina Faso; rais wa Seneti ya Misri; katibu mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Palestina ya Jihad Islami; na spika wa bunge la Oman.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, viongozi wengine waandamizi waliokuwepo ni pamoja na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai Nurlan Yermekbayev, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya D-8 ya Ushirikiano wa Kiuchumi, na Naibu Katibu Mkuu wa Shirika la Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).

Wengine waliohudhuria ni pamoja na naibu mwenyekiti wa baraza la kisiasa la Hizbullah; Makamu wa Rais wa Uturuki Cevdet Yılmaz; Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Waleed El Khereiji; mkuu wa baraza la uongozi la Hamas; waziri wa mambo ya nje wa Kazakhstan; Waziri wa Ulinzi wa Lebanon Michel Mnassa; Mwenyekiti wa Seneti ya Pakistan Syed Yousaf Raza Gilani; Waziri wa Elimu ya Juu wa Cuba Walter Baluja García; Waziri wa Masuala ya Ikulu wa Namibia Charles Mubita; Spika wa Baraza la Shura la Qatar; Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Watu la China He Wei; pamoja na Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Urusi Dmitry Medvedev. Wajumbe maalum kutoka Serbia, Myanmar, Malaysia, Tanzania na Thailand nao pia walihudhuria..

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei alinukuliwa akisema kuwa wajumbe kutoka takriban nchi 100, pamoja na watu maarufu na makundi ya jamii za kiraia, walihudhuria hafla ya jana.

Ripoti hiyo ilieleza kuwa hafla hiyo ni miongoni mwa mikusanyiko mikubwa zaidi ya kimataifa nchini Iran katika kipindi cha hivi karibuni, ikidhihirisha heshima na mvuto aliokuwa nao Kiongozi Shahidi katika nyanja za siasa, dini na utamaduni.

Kwa mujibu wa maafisa wa Iran, mazishi ya siku kadhaa yanatarajiwa kuvuta waombolezaji kati ya milioni 15 hadi 20.

Shughuli za mazishi zitaendelea Jumamosi,  Jumapili na Jumatatu jijini Tehran. Ratiba nyingine imepangwa katika mji mtakatifu wa Qom, ikifuatiwa na kisha katika miji ya Karbala na Najaf nchini Iraq, kabla ya maziko Mashhad, kaskazini mashariki mwa Iran tarehe 9 Julai.