Mazishi ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu yaanza Tehran
-
Mwili mtoharifu wa Kiongozi Shahidi na watu wa familia yake ambap waliuawa shahidi pamoja naye
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeanza awamu ya kwanza ya taratibu za mazishi ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, huku viongozi wa kimataifa na wanazuoni wa kidini wakifika katika Ukumbi wa Sala wa Imam Khomeini maarufu kama Mosalla mjini Tehran kutoa heshima zao za mwisho.
Mwili wa Kiongozi huyo, pamoja na wanafamilia wake, ulipelekwa katika Ukumbi wa Sala wa Imam Khomeini kwa ajili ya maombolezo ya hadhara ya siku mbili.
Wanazuoni wa kidini na watu mashuhuri wa kitamaduni kutoka Indonesia, Iraq, Lebanon, Yemen, Pakistan na Afghanistan walikuwa miongoni mwa wageni wa kwanza wa kimataifa kufika kutoa heshima. Wawakilishi wa jamii za dini wachache wanaotambuliwa rasmi nchini Iran pia walihudhuria shughuli hiyo kumuenzi Kiongozi huyo marehemu.
Maafisa wa ngazi za juu na wawakilishi kutoka nchi zaidi ya 30, zikiwemo Russia, China, Pakistan, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Armenia, Uturuki, India, Georgia, na Cuba, wamewasili Iran kuhudhuria mazishi hayo kufuatia mauaji ya kigaidi ya Ayatullah Khamenei yaliyotekelezwa na Marekani na utawala wa Kizayuni katika siku ya kwanza ya vita vya hivi karibuni vya siku 40.
Maombolezo ya hadhara yaliyoanza Ijumaa yanafuatia shughuli ya faragha iliyofanyika Alhamisi jioni, ambapo familia za mashahidi wa vita vya hivi karibuni na jamaa za wafanyakazi wa ofisi ya Kiongozi walikusanyika kutoa buriani zao za mwisho.
Rais Masoud Pezeshkian ametoa wito kwa Wairani kutoka matabaka yote kujitokeza kwa wingi.
Rais aliandika katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X kwamba, “Wakati Iran yenye ushujaa ikijitayarisha kumuaga mtumishi mwaminifu wa Uislamu na Mapinduzi, nawaalika wananchi wote, bila kujali kabila, dini, mwelekeo wa kisiasa au itikadi, kushiriki kwa hamasa, heshima, na idadi kubwa ya kihistoria; ili kuonyesha taswira ya kudumu ya umoja wa kitaifa na uaminifu kwa malengo matukufu ya mfumo wa Kiislamu.”
Kwa mujibu wa maafisa wa Iran, mazishi hayo ya siku kadhaa yanatarajiwa kuvutia waombolezaji kati ya milioni 15 na 20.
Taratibu zitaendelea Jumamosi na Jumapili mwili ukiwa umewekwa hadharani katika Mosalla kabla ya maandamano makubwa ya mazishi kuzunguka Tehran siku ya Jumatatu. Ibada zaidi zimepangwa katika mji mtakatifu wa Qom, zikifuatiwa na shughuli nyingine Karbala, Kufa na Najaf nchini Iraq, kabla ya maziko ya mwisho huko Mashhad, Kaskazini Mashariki mwa Iran katika Haram Tukufu ya Imam Ridha (AS) mnamo Julai 9.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, shughuli hiyo ya mazishi leo inahudhuriwa na wageni kutoka takriban nchi 100, wakiwemo wakuu wa nchi, maspika wa mabunge, mawaziri wa mambo ya nje, wawakilishi maalum wa serikali, pamoja na watu mashuhuri wa nyanja za kisiasa, kidini, kitamaduni, na makundi mbalimbali ya kijamii.
Kuanzia saa 8:00 mchana leo, maafisa wa ngazi za juu kutoka nchi mbalimbali na watu mashuhuri wa kisiasa wameshiriki katika shughuli hiyo ili kutoa heshima na buriani zao za mwisho kwa mwili wa Kiongozi huyo Shahidi.
Ayatullah Seyyed Ali Khamenei aliuawa shahidi akiwa na baadhi ya watu wa familia yake katika shambulio la Marekani na Israel dhidi ya ofisi yake mjini Tehran mnamo 10 Ramadhani 1447 Hijria Qamaria sawa Februari 28, 2026, mwanzoni mwa vita vya uchokozi vya siku 40 dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Masuala ya Kisheria na Kimataifa, Kazem Gharibabadi, amesema kuwa kumbukumbu ya kuangushwa kwa ndege ya abiria ya Iran Air 655 na kuombolezwa kwa Kiongozi huyo wote ni dhihirisho la uadui wa kudumu wa Marekani dhidi ya taifa la Iran.
“Siku hizi, sambamba na kuwakumbuka mashahidi wa Flight 655, taifa la Iran pia linaenzi kumbukumbu ya Kiongozi wake Shaheed,” aliandika kwenye X, akiongeza kuwa kuuwawa kwa Kiongozi huyo ni ishara ya “mwendelezo na kina cha uadui wa Marekani dhidi ya taifa la Iran” na pia “ustahimilivu wa kudumu wa wananchi wa Iran.”
Iran huadhimisha Julai 3 kama kumbukumbu ya kuangushwa kwa ndege ya Iran Air 655 mnamo 1988 na meli ya kivita ya USS Vincennes juu ya Ghuba ya Uajemi, maafa yaliyopelekea vifo vya watu wote 290 waliokuwemo, wakiwemo watoto 66. Maafisa wa Iran wamekuwa wakikemea vikali Marekani kwa kukataa kuomba radhi rasmi na baadaye kuipongeza kwa medali kamanda wa meli hiyo ya kivita.