Qalibaf ageuza diplomasia ya mazishi kuwa jukwaa la shughuli za kikanda
Marasimu ya mazishi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyeuawa shahidi, Ayatollah Seyyed Ali Khamenei, yamekuwa zaidi ya shughuli ya maombolezo ya kitaifa. Mazishi haya yameipa Iran fursa kubwa ya kidiplomasia, huku viongozi wakuu na jumbe za ngazi za juu kutoka kote Asia na Mashariki ya Kati wakikusanyika mjini Tehran kwa ajili ya kujadili masuala ya usalama wa kikanda, diplomasia ya baada ya vita na ushirikiano wa kimkakati.
Mhimili wa mazungumzo haya ni Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Bunge la Iran ambaye amekutana pambizoni mwa mazishi haya na viongozi wa ngazi za juu wa nchi mbalimbali wakiwemo wa China, Iraq, Belarus, Bangladesh, Lebanon, na jimbo la Kurdistan ya Iraq. Majadiliano hayo yamelenga utekelezaji wa mkataba wa maelewano kati ya Iran na Marekani (MoU) uliofikiwa hivi karibuni, utulivu wa eneo, na kuimarishwa uhusiano wa kisiasa na kibunge.
Suala lililojirudia katika mikutano hiyo ni kuhusu usimamizi wa baadaye wa Lango-Bahari la Hormuz kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano. Katika mazungumzo yake na He Wei, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Kitaifa la Watu wa China, na vile vile Haibat al-Halbousi Spika wa Bunge la Iraq, Qalibaf amesema Iran inashauriana na nchi jirani za pwani ya Ghuba ya Uajemi kuhusu utekelezaji wa mipango ya baharini iliyomo katika hati ya makubaliano hayo. Amesisitiza kwamba, chini ya sheria ya kimataifa, jukumu la kusimamia njia hiyo ya ya kimkakati ya baharini ni la Iran na Oman, na kukariri tena kwamba Tehran haitakubali ushiriki wowote wa Marekani katika suala hilo.
Ameituhumu Israel kwa kujaribu kuvuruga makubaliano ya Iran na Marekani, na kusema nguvu ya kuzuia hujuma ya Tehran utazuia mzozo wowote mpya wa kijeshi. Huku akithibitisha tena msimao wa Iran wa kuheshimu makubaliano hayo, ameonya kwamba Tehran itachukua "hatua zinazofaa na zenye uwiano" ikiwa Washington au Israel zitakataa kutekeleza majukumu yao.
Katika vikao vyake vyote, spika wa bunge la Iran amesema mzozo wa hivi karibuni umethibitisha mapungufu ya mashinikizo ya kijeshi dhidi ya Iran, na kwamba kusitishwa mapigano hatimaye kulitokana na uwezo wa kujilinda wa Iran na mbinu yake ya diplomasia.
Kupanuliwa ushirikiano wa kikanda imekuwa mada nyingine muhimu ya mashauriano hayo ya kidiplomasia. Wakati wa kikao chake na ujumbe wa China, Qalibaf ametaka kuwepo na uratibu wa kimkakati wa karibu zaidi kati ya Tehran na Beijing, na kuelezea ushirikiano imara wa kisiasa, kiuchumi, na kibunge kama suala muhimu sana, katika kivuli cha mabadiliko ya kimienendo, kikanda na kimataifa. Amesisitiza ushirikiano kufanyika ndani ya jumuiya za pande kadhaa kama vile BRICS na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai kama njia bora zaidi ya kuimarisha utulivu na kukabiliana na siasa za upande mmoja.
Viongozi wa China wamesisitiza tena kujitolea kwa Beijing katika kuimarisha ushirikiano wake wa kimkakati na Iran, wakibainisha kuwa mwaka huu unatimiza miaka 55 ya uhusiano wa kidiplomasia na miaka kumi ya ushirikiano wa kimkakati wa nchi mbili hizi.
Katika mazungumzo tofauti na Halbousi, Spika wa Bunge la Iraq, pande zote mbili zimesisitiza uhusiano wa kina wa kihistoria, kisiasa, na kidini kati ya nchi hizi jirani. Halbousi ameipongeza Iran kwa 'mafanikio yake katika mzozo wa karibuni' na kukaribisha makubaliano ya maelewano, akielezea matumaini kwamba yatachangia pakubwa katika utulivu wa kikanda na kuwezesha kuanza tena kwa mauzo ya nje ya nishati kupitia Lango-Bahari la Hormuz. Qalibaf pia amekutana na kuzungumza na Nechirvan Barzani, Rais wa Jimbo Lenye Utawala wa Ndani la Kurdistan ya Iraq, ambapo majadiliano yalilenga ushirikiano wa pande mbili na usalama wa kikanda. Akisisitiza tena mbinu ya Iran kuhusu diplomasia, Qalibaf amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran "hujadiliana kwa mantiki na kusimama dhidi ya mabavu," na kukariri tena azma ya Tehran ya kutetea maslahi yake ya kitaifa.
Vikao vya Igor Sergeenko Spika wa Baraza la Wawakilishi la Belarusi na ujumbe wa Lebanon uliomwakilisha Spika wa Bunge Nabih Berri pia vililenga kuimarisha ushirikiano miongoni mwa nchi zinazopinga mabavu na siasa za upande mmoja kufuatia mzozo wa kikanda wa hivi karibuni.
Sergeenko amekariri tena uungaji mkono wa Belarusi kwa Iran, akilaani mashambulizi dhidi ya miundombinu ya raia na kuelezea utayari wa Minsk wa kupanua ushirikiano na Tehran katika mifumo ya kisiasa, kiuchumi, kibunge, na ya pande nyingi.
Katika mkutano wake na ujumbe wa Lebanon, Qalibaf amesema kulindwa umoja wa Waislamu na kukabiliana na siasa kandamizi za tawala za kigeni ni urithi aliotuachia Kiongozi Mkuu wa Iran aliyeuawa shahidi na maadui wa ubinadamu. Pia amesema Lebanon imekuwa suala muhimu wakati wa mazungumzo ya kutatua mzozo wa hivi karibuni, huku Tehran ikisisitiza juu ya vifungu vinavyolenga kulinda utulivu na uthabiti wa Lebanon. Hafiz Uddin Ahmad, Spika wa Bunge la Bangladesh pia amekutana na Qalibaf kando ya mazishi haya, na kuashiria ushiriki mkubwa wa kimataifa katika tukio hili ambalo limevutia wajumbe wengi rasmi kutoka kote Asia, Mashariki ya Kati, na kwingineko.
Amesifu juhudi za Tehran za kutumia mazishi haya kama jukwaa la diplomasia ya kikanda na kimataifa. Sambamba na kumuenzi Kiongozi aliyeuawa shahidi, maafisa wa Iran wametumia vizuri fursa hii kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano wa kimkakati, kupanua mazungumzo na mataifa jirani, na kuendeleza dira ya usalama wa kikanda inayohusu ushirikiano kati ya madola ya kikanda, ushirikiano wa pande nyingi, na kupunguza uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya eneo.