Lebanon yakanusha madai ya kuwepo silaha katika ngome ya Hizbullah
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i127368-lebanon_yakanusha_madai_ya_kuwepo_silaha_katika_ngome_ya_hizbullah
Jeshi la Lebanon linasema kuwa limekamilisha oparesheni zake za ukaguzi wa silaha na zana za kijeshi katika kitongoji cha Dahiyeh, kusini mwa Beirut, ngome ya Harakati ya Muqawama ya Hizbullah, bila kupata chochote cha kutia shaka.
(last modified 2025-06-09T11:12:23+00:00 )
Jun 09, 2025 11:12 UTC
  • Lebanon yakanusha madai ya kuwepo silaha katika ngome ya Hizbullah

Jeshi la Lebanon linasema kuwa limekamilisha oparesheni zake za ukaguzi wa silaha na zana za kijeshi katika kitongoji cha Dahiyeh, kusini mwa Beirut, ngome ya Harakati ya Muqawama ya Hizbullah, bila kupata chochote cha kutia shaka.

Jeshi hilo limesema katika taarifa yake kuwa, limefanya ukaguzi huo katika mitaa ya al-Marija na Laylaki katika wilaya ya Dahiyeh kufuatia mwongozo wa kamati ya Umoja wa Mataifa ya kufuatilia usitishaji vita, ambayo ilionya kuwa eneo hilo lingeshambuliwa kwa mabomu iwapo silaha zingelikuwepo.

Awali jeshi la Lebanon lilipinga ombi hilo, likitaja uwezo mdogo wa kamati hiyo katika maeneo ya kusini mwa Mto Litani. Hata hivyo, kamati hiyo ilihimiza kufanyika msako wa kina, ikiomba kuchimba hadi mita 10 kwenda chini, kwa tuhuma za kuwepo vituo vya chini ya ardhi ambavyo vinaweza kukiuka masharti ya kusitisha mapigano.

Ukaguzi huo umekuja baada ya ndege za kivita za Israel kuanzisha wimbi la mashambulizi ya anga katika vitongoji vya kusini mwa Beirut, yakilenga vitongoji vilivyo na watu wengi vya Hadath, Haret Hreik, na Burj al-Barajneh, katika mkesha wa sikukuu ya Iddul al-Adh'ha.

Mnamo Januari 27, 2025, Lebanon ilikuwa imetangaza uamuzi wake wa kurefusha muda wa usitishaji vita na Israel hadi Februari 18. Hata hivyo, tangu kuanza kwa utekelezaji wa usitishaji vita, vikosi vya Israel vimekuwa vikikiuka makubaliano hayo mara kwa mara kwa kuanzisha mashambulizi katika ardhi ya Lebanon, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya anga kote nchini humo.

Chini ya masharti ya makubaliano ya kusitisha mapigano, Israel ililazimika kuondoka kikamilifu kusini mwa Lebanon ifikapo Januari 26. Makataa hayo yaliongezwa hadi Februari 18, lakini Tel Aviv imekataa kuyaheshimu. Hadi leo, Israeli inadumisha uwepo wa kijeshi kwenye vituo vitano vya mpaka vya Labbouneh, Mount Blat, Owayda Hill, Aaziyyeh, na Hammamis.