EU yataka kufunguliwa korido ya kibinadamu mashariki mwa Kongo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i132870-eu_yataka_kufunguliwa_korido_ya_kibinadamu_mashariki_mwa_kongo
Afisa wa Umoja wa Ulaya ametoa wito kwa pande husika katika mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufungua koridi ya kibinadamu na kuruhusu kuanza kuingia kwa ndege za misaada ya kibinadamu.
(last modified 2025-11-06T11:09:30+00:00 )
Nov 06, 2025 11:09 UTC
  • Johan Borgstram akizungumza na waandishi wa habari mjini Kinshasa
    Johan Borgstram akizungumza na waandishi wa habari mjini Kinshasa

Afisa wa Umoja wa Ulaya ametoa wito kwa pande husika katika mzozo wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufungua koridi ya kibinadamu na kuruhusu kuanza kuingia kwa ndege za misaada ya kibinadamu.

Akihutubia mkutano wa waandishi wa habari katika mji mkuu Kinshasa, Johan Borgstram, Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Ulaya katika eneo la Maziwa Makuu ,amesema amesikitishwa na kuharibiwa huduma muhimu katika eneo hilo na kutoa wito kwa pande zinazozozana "kuheshimu kanuni za sheria za kimataifa za kibinadamu."

Borgstarm amewalaumu waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda kwa kuchochea mzozo wa mashariki mwa Kongo ambao umesababisha maelfu ya raia kuwa wakimbizi. 

Mwakilishi Maalumu wa Umoja wa Ulaya katika eneo la Maziwa Makuu pia amekosoa kile kinachodaiwa kuwa  uwepo wa wanajeshi wa Rwanda huko Kongo, akisema ni ukiukaji mamlaka ya kujitawala ya Kongo.

Johan Borgstram wakati huo huo amepongeza juhudi za wasuluhishi katika mazungumzo kati ya serikali ya Kongo na waasi na kusisitiza kuwa ipo haja kwa pande zote husika katika mgogoro wa Kongo kuheshimu makubaliano ya kustisha vita na kujikita katika mazungumzo ya dhati. 

Itakumbukwa kuwa, waasi wa kundi la Machi 23 (M23) Julai mwaka huu walisaini mkataba wa Azimio la Kanuni kwa ajili ya kusitisha mapigano mashariki mwa Kongo. 

Hata hivyo mapigano yanaendelea kati ya askari jeshi wa serikali ya Kinshasa na kundi la M23, huku kila upande ukihutumu mwingine kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano. 

Ripoti ya serikali ya Kongo inaonyesha kuwa watu karibu milioni 7 wamekuwa wakimbizi wa ndani nchini humo.

Waasi wa M23 wiki iliyopita walidai kuwa "hakuna tena dharura yoyote ya kibinadamu" katika maeneo wanayodhibiti, "kwa kuwa watu wote waliokimbia makazi yao wamerejea katika maeneo yao ya asili."