ICRC: Mgogoro wa afya Kongo DR unazidi kuwa mbaya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131766-icrc_mgogoro_wa_afya_kongo_dr_unazidi_kuwa_mbaya
Mfumo wa huduma za afya katika eneo linalokumbwa na migogoro mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) umezorota kwa kiasi kikubwa, huku vituo vingi vya matibabu vikiwa na uhaba mkubwa wa dawa na wafanyakazi, Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imeonya katika taarifa yake ya jana Jumatano.
(last modified 2025-10-08T23:41:34+00:00 )
Oct 08, 2025 23:41 UTC
  • ICRC: Mgogoro wa afya Kongo DR unazidi kuwa mbaya

Mfumo wa huduma za afya katika eneo linalokumbwa na migogoro mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) umezorota kwa kiasi kikubwa, huku vituo vingi vya matibabu vikiwa na uhaba mkubwa wa dawa na wafanyakazi, Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imeonya katika taarifa yake ya jana Jumatano.

Utafiti wa ICRC uliofanyika mwezi uliopita wa Septemba katika vituo vya afya 240 katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini uligundua kuwa, asilimia 85 ya vituo hivo havina dawa muhimu, huku karibu asilimia 40 vilisema wafanyakazi wa afya wamekimbia kutokana na ukosefu wa usalama na uhaba wa fedha.

Uhaba huo unawalazimu raia waliojeruhiwa, wakiwemo wanawake na watoto, kusafiri masafa marefu kwa ajili ya kusaka matibabu, mara nyingi wakilazimika kupitia maeneo ya vita, imeongeza ICRC.

Hippolyte Ten, Naibu Mratibu wa Afya wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu ICRC ameeleza bayana kuwa, "Hata wagonjwa wanapofanikiwa kufika kliniki, mara nyingi hawapati wafanyakazi waliohitimu au dawa wanazozihitaji."

Zaidi ya asilimia 70 ya vituo vilivyochunguzwa vilitibu majeraha yanayohusiana na silaha mwaka huu, huku hospitali za Beni, Goma, Bukavu, na Fizi zikiripoti zaidi ya kesi 3,400, likiwa ni ongezeko la asilimia 160 kutoka mwaka 2024. ICRC pia ilirekodi kesi 948 za unyanyasaji wa kingono zilizopokea usaidizi wa kimatibabu na kisaikolojia katika nusu ya kwanza ya mwaka huu 2025.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW) lilieleza karibuni kuwa, waasi wa kundi la M23 wameuwa makumi ya raia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.