UN: Wanawake wa Sudan wanakabiliwa na mashambulizi wakitafuta maji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140192-un_wanawake_wa_sudan_wanakabiliwa_na_mashambulizi_wakitafuta_maji
Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women) limetangaza kwamba wanawake na wasichana katika eneo la al-Obeid nchini Sudan wanakabiliwa na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na ukatili wa kingono wanapokuwa katika jitihada za kupata maji huku hali ya kibinadamu ikizidi kuwa mbaya.
(last modified 2026-07-27T03:52:18+00:00 )
Jul 27, 2026 03:50 UTC
  • UN: Wanawake wa Sudan wanakabiliwa na mashambulizi wakitafuta maji

Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women) limetangaza kwamba wanawake na wasichana katika eneo la al-Obeid nchini Sudan wanakabiliwa na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na ukatili wa kingono wanapokuwa katika jitihada za kupata maji huku hali ya kibinadamu ikizidi kuwa mbaya.

Ripoti ya shirika hilo la Umoja wa Mataifa imesema kwamba raia katika mji huo uliozingirwa wanasumbuliwa na hali mbaya, wakati mapigano kati ya jeshi la Sudan na wapiganaji wa Rapid Support Forces (RSF) yakizidi kuwa makali.

El-Obeid, mji mkuu wa jimbo la Kordofan Kaskazini, inasumbuliwa na uhaba mkubwa wa chakula, huduma za afya na maji safi, huku maafisa wa Umoja wa Mataifa wakionya kwamba mgogoro mkubwa wa binadamu unajitokeza katika eneo hilo.

Anna Mutavati, Mkurugenzi wa Kanda wa Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, amesema wanawake na wasichana huko El-Obeid wamefanyiwa unyanyasaji, ubakaji na aina nyingine za unyanyasaji wa kingono wakati wakijaribu kupata maji.

"Wanawake na wasichana hawa wamenyanyaswa. Wamebakwa, na wamefanyiwa aina nyingine za ukatili wa kingono, wakijaribu kupata maji ambayo ni mojawapo ya mahitaji muhimu zaidi ya maisha," amesema Mutavati akiwaambia waandishi wa habari mjini Geneva kupitia kiungo cha video kutokea Nairobi.

Kwa mujibu wa Shirika la Wanawake la Umoja wa Mataifa, wanawake na wasichana wanaofanya jitihada za kupata maji hawako salama huko El Obeid. Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yanayolenga vyanzo vya maji nyakati za mchana yamewalazimisha wakazi wengi kuteka maji baada ya giza kuingia, na kuwaweka wanawake na wasichana katika hatari zaidi za unyanyasaji wa kingono.

Wakati huo huo Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk amesema raia huko El-Obeid nchini Sudan wamevumilia hali inayofanana na ya kuzingirwa kwa miezi 18, ikiambatana na uhaba mkubwa wa maji safi na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani.

Turk ameonya kwamba hali hiyo inaweza kupelekea kukaririwa ukatili ulioshuhudiwa huko El Fashir huko Darfur Kaskazini, mwaka jana.

Vita nchini Sudan, ambavyo sasa vinaingia mwaka wake wa nne, vimesababisha mojawapo ya migogoro mikubwa zaidi ya binadamu duniani, huku visa vingi vya unyanyasaji wa kingono na unyanyasaji mwingine zikiendelea kuwaathiri raia.

UN Women imesema takriban wanawake na wasichana milioni 12.7 kote Sudan wanatarajiwa kuhitaji huduma zinazohusiana na matatizo ya unyanyasaji wa kingono mwaka huu, likiwa ni ongezeko mara nne tangu kuanza kwa vita vya ndanii nchini Sudan.