Qalibaf: Iran na Pakistan zinatoa kipaumbele kwa uhusiano wa kiuchumi na kibiashara
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i132876-qalibaf_iran_na_pakistan_zinatoa_kipaumbele_kwa_uhusiano_wa_kiuchumi_na_kibiashara
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema kuwa kupanua uhusiano wa kiuchumi na kuzidisha kiwango cha biashara kati ya Tehran na Islamabad ni vipaumbele vya juu vya nchi zote mbili.
(last modified 2025-11-06T11:14:00+00:00 )
Nov 06, 2025 11:14 UTC
  • Spika wa Bunge la Iran ziarani Pakistan
    Spika wa Bunge la Iran ziarani Pakistan

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema kuwa kupanua uhusiano wa kiuchumi na kuzidisha kiwango cha biashara kati ya Tehran na Islamabad ni vipaumbele vya juu vya nchi zote mbili.

Mohammad Bagher Qalibaf amebainisha haya leo mjini Islamabad katika mkutano na Ayaz Sadiq Spika wa Bunge la Taifa la Pakistan. 

Spika wa Bunge la Iran amesema amefurahiswa na ziara yake nchini Pakistan na kusema: Tunashukuru wananchi wa Pakistan kwa uungaji mkono wao kwa wananchi wa Iran  dhidi ya uvamizi wa utawala wa Kizayuni. Ungaji mkono huu unadhihirisha uhusiano mkubwa na wa kirafiki uliopo kati ya watu wa Iran na Pakistan.  

Mohammad Bagher Qalibaf pia amesisitiza kuwa mshikamano ulioonyeshwa na nchi hizo mbili katika nyakati ngumu unaakisi uhusiano mkubwa uliopo kati ya Tehran na Islamabad na kusema: Ana tumai kuwa  ziara yake nchini Pakistan itaimarisha uhusiano kati ya nchi mbili hususan uhusiano baina ya mabunge. 

Katika mazungumzo hayo, mwenyeji wa Qalibaf, Ayaz Sadiq Spika wa Bunge la Taifa la Pakistan amesema: Bunge la Pakistan lililaani mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran na kupasisha azimio lililoeleza kuwa:" Kwa mtazamo wetu, Israel ni adui wa pamoja wa Iran na Pakistan.”

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran pia amekutana na kuzungumza na Sayyid Yousuf Raza Gilani Mwenyekiti wa Seneti ya Pakistan ambaye pia ni Kaimu Rais wa Pakistan.