Google yafuta ushahidi wa video za uhalifu wa Israel huko Palestina
-
Google; mshirika katika jinai za Israel
Nyaraka zilizopatikana zinaonyesha kwamba kampuni ya Kimarekani ya Google imefuta zaidi ya video 700 zinazoonyesha uhalifu wa kivita wa utawala wa Israel kutoka kwenye mtandao wa intaneti.
Katika mwendelezo wa himaya na uungaji mkono wa makampuni ya teknolojia ya Marekani kwa uhalifu wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina, sasa kuna habari za kufutwa ushahidi wa video wa uhalifu uliofanywa na Israel kwenye vita vya Gaza.
Gazeti la Middle East Spectator limeripoti mapema leo Alkhamisi kwamba: "Tangu mwanzoni mwa Oktoba kampuni ya Google imefuta zaidi ya video 700 zinazoonyesha uhalifu wa kivita wa Israel kutokana na mashinikizo ya utawala wa Trump."
Ripoti hiyo inasema: "Video zilizofutwa zinajumuisha picha za mauaji ya Shireen Abu Akleh, mwandishi wa habari wa televisheni ya Al Jazeera ambaye alikuwa raia wa Marekani na ambaye maafisa wa Marekani wanaamini alipigwa risasi kwa makusudi na jeshi la Israel."
Chombo hicho cha habari, kimepitia nyaraka zilizovuja na kuandika kuwa: "Google pia ilisaini mkataba wa dola milioni 45 kwa ajili ya kuchapisha propaganda za Israel wakati wa kilele cha njaa ya makusudi huko Gaza na kwa ajili ya kuhalalisha uchokozi dhidi ya Iran."
Ripoti ya Middle East Spectator inahitimisha kwamba: "Barua pepe za ndani zinaonyesha kwamba Google imepinga mara kwa mara kwamba matangazo ya Israel yanayokana kuwepo njaa ya makusudi huko Gaza yanakiuka sera zake."