Waangalizi wa AU: Uchaguzi wa Tanzania haukukidhi viwango vya kimataifa
-
Uchaguzi mkuu Tanzania
Ujumbe wa waangalizi wa Umoja wa Afrika katika uchaguzi mkuu wa wiki iliyopita nchini Tanzania uliogubikwa na ghasia umeeleza kuwa uchaguzi huo haukukidhi viwango vya kimataifa vya kidemokrasia.
Taasisi hiyo ya barani Afrika jana ilieleza kuwa waangalizi wa uchaguzi waliona wapiga kura wakipewa karatasi nyingi za kupigia kura na kujazwa kwenye masanduku ya kura.
Taarifa ya ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi wa Umoja wa Afrika imeongeza kuwa: Wawakilishi wake kadhaa wa ujumbe katika tmu ya wasangalizi wa uchaguzi walitakiwa kuondoka katika vituo vya kupigia kura, kabla ya mchakato wa kuhesabu kura kukamilika.
Taarifa hiyo ya waangalizi wa uchaguzi wa AU imeendelea kubainisha: Vyombo vya habari viliathiriwa na vizuizi wakati wa maandalizi ya uchaguzi huku mashirika ya haki za kiraia yakizuiwa pia kutoa elimu kwa wapiga kura.
"Huduma ya intaneti ilisitishwa siku ya uchaguzi na baadaye pia hakukuwa na intaneti; hatua iliyohatarisha uadilifu kwa mchakato wa uchaguzi.
Serikali ya Tanzania kwa upande wake imesema kuwa uchaguzi ulikuwa wa haki na wa uwazi. Rais Samia Suluhu Hassan ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa Oktoba 29 ulioambatana na ghasia kubwa. Wapinzani nchini Tanzania wanaituhumu serikali kwa udanganyifu na kupotea kwa maisha ya watu wakati wa maandamano ya baada ya uchaguzi.