Tanzania kuanza kujenga bandari yenye thamani ya dola bilioni 10 mwezi Desemba
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133554-tanzania_kuanza_kujenga_bandari_yenye_thamani_ya_dola_bilioni_10_mwezi_desemba
Tanzania itaanza ujenzi wa bandari mpya mashariki mwa nchi mwezi Desemba mwaka huu na hivyo kumaliza muongo mmoja wa ucheleweshaji kutokana na pingamizi la serikali kwa masharti ya awali ya kandarasi.
(last modified 2025-11-24T15:14:07+00:00 )
Nov 24, 2025 15:14 UTC
  • Gerson Msigwa
    Gerson Msigwa

Tanzania itaanza ujenzi wa bandari mpya mashariki mwa nchi mwezi Desemba mwaka huu na hivyo kumaliza muongo mmoja wa ucheleweshaji kutokana na pingamizi la serikali kwa masharti ya awali ya kandarasi.

Bandari ya Bagamoyo, ambayo ni sehemu ya mpango mkubwa wa eneo maalumu la kiuchumi unaohusisha bustani za viwanda na viunganishi vya reli na barabara, iko umbali wa takriban kilomita 75 kaskazini mwa mji mkuu wa kibiashara, Dar es Salaam.

Gerson Msigwa msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania amewaambia waandishi wa habari kuwa bandari ya Bagamoyo itakuwa na gati 28, lakini ujenzi utaanza Desemba 14. 

Msigwa amesema mitambo ya ujenzi ipo njiani na kwamba bandari hiyo itakuwa na kina cha hadi mita 20 na itakuwa na uwezo wa kupokea meli kubwa kuliko bandari yoyote katika ukanda wa Afrika Mashariki.

"Bandari hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia meli zenye uwezo wa kubeba hadi makontena 25,000,” amesema Msigwa.

Taifa hilo la Afrika Mashariki lilitia saini makubaliano ya mfumo na kampuni za ujenzi kutoka China na Oman mwaka 2013 lakini utekelezaji ulicheleweshwa kwa sababu serikali ilisema masharti hayo hayakuwa mazuri kwa nchi.

Baada ya kula kiapo mwaka 2021, Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania alisema kuwa walikuwa wameanza mazungumzo ya kufufua mradi huo wa dola bilioni 10.