Rais Samia: Ghasia za uchaguzi zinaweza kuathiri upatikanaji wa fedha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i133358-rais_samia_ghasia_za_uchaguzi_zinaweza_kuathiri_upatikanaji_wa_fedha
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania jana alisema kuwa ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi wa Oktoba 29 zinaweza kuathiri upatikanaji wa ufadhili wa kimataifa kwa nchi hiyo.
(last modified 2025-11-19T06:58:36+00:00 )
Nov 19, 2025 06:58 UTC
  • Rais Samia: Ghasia za uchaguzi zinaweza kuathiri upatikanaji wa fedha

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania jana alisema kuwa ghasia zilizotokea baada ya uchaguzi wa Oktoba 29 zinaweza kuathiri upatikanaji wa ufadhili wa kimataifa kwa nchi hiyo.

Rais Samia alisema katika hafla ya kuwaapisha Mawaziri wateule wa serikali yake kwamba kilichotokea kimechafua taswira ya nchi na kupunguza nafasi zake za kupata mikopo.

Amewataka maafisa wa serikali kujikita katika kutafuta fedha za maendeleo vyanzo vikiwa ni rasilimali za ndani. 

Tanzania bado inategemea kifedha ufadhili wa nchi za nje ambapo mwaka 2023  misaada hiyo ilichangia takriban asilimia 23 ya mapato ya serikali.

Uchaguzi mkuu wa Tanzania wa Oktoba 29 mwaka huu ulikumbwa na maandamano ya ghasia na fujo baada ya siku tatu za makabiliano kati ya waandamanaji na polisi. 

Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ijumaa tarehe 14 mwezi huu alitoa msamaha kwa vijana waliofanya fujo wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 akisema kuwa, walifuata mkumbo na hawakujua walifanyalo.

Rais Samia alitoa maelekezo maalumu kwa vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania, hususan Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kuchuja upya mashitaka yanayowakabili vijana walioshtakiwa kwa makosa ya uhaini kufuatia fujo zilizofanyika wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 nchini humo.