Araghchi: Iran, US kufanya mazungumzo ya nyuklia Muscat
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i136270-araghchi_iran_us_kufanya_mazungumzo_ya_nyuklia_muscat
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi ametangaza kwamba mazungumzo ya nyuklia kati ya Jamhuri ya Kiislamu na Marekani yanatazamiwa kufanyika katika mji mkuu wa Oman, Muscat kesho asubuhi.
(last modified 2026-02-05T02:56:00+00:00 )
Feb 05, 2026 02:56 UTC
  • Araghchi: Iran, US kufanya mazungumzo ya nyuklia Muscat

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi ametangaza kwamba mazungumzo ya nyuklia kati ya Jamhuri ya Kiislamu na Marekani yanatazamiwa kufanyika katika mji mkuu wa Oman, Muscat kesho asubuhi.

Katika ujumbe uliotumwa kwenye mtandao wa kijamii wa X, mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amesema mazungumzo hayo yamepangwa kufanyika Ijumaa saa nne asubuhi hivi, akiishukuru Oman kwa kuweka mazingira yanayohitajika kwa ajili ya mkutano huo.

Hapo awali, ripoti za vyombo vya habari vya Iran zilisema, mazungumzo hayo yatajikita juu ya mpango wa amani wa nishati ya nyuklia wa Iran pekee, na kuondolewa kwa vikwazo, pasi na kujadiliwa masuala mengine.

Sayyid Araghchi anatarajiwa kuongoza ujumbe wa Iran ambao utajumuisha wanadiplomasia wakuu Majid Takht-Ravanchi na Kazem Gharibabadi kwenye mazungumzo hayo. Marekani kwa upande wake itawakilishwa na Mjumbe Maalum wa Ikulu ya White House Steve Witkoff, kwa mujibu wa ripoti hizo.

Habari zaidi zinasema kuwa, mazungumzo hayo yatafanyika kwa njia isiyo ya moja kwa moja, huku Oman ikiwa mpatanishi.

Awali, duru hii mpya ya mazungumzo ilipangwa kufanyika Istanbul nchini Uturuki, lakini imehamishiwa Muscat, mji mkuu wa Oman kwa ombi la Iran.

Muundo wa mazungumzo hayo utafanana na duru za awali zilizofanyika kabla ya vita vya kutwisha vilivyoanzishwa na Israel na Marekani dhidi ya Iran mwezi Juni mwaka jana, ambavyo vilivuruga mchakato huo wa kidiplomasia.