Lengo jipya la mkakati wa kijeshi wa Marekani barani Afrika
Kamandi ya Marekani barani Afrika (AFRICOM) imetangaza kupeleka kikosi kidogo cha kijeshi cha Marekani nchini Nigeria na hivyo kwa mara ya kwanza kukiri rasmi kutumwa wanajeshi wa Marekani katika nchi hiyo ya Afrika.
Akizungumzia ukweli kwamba kikosi kidogo cha kijeshi cha Marekani tayari kimepekwa nchini Nigeria, Jenerali Dagwin Anderson, kamanda wa kamandi ya Africom amesema: 'Kutumwa kwa kikosi hiki kumefanyika ndani ya muafaka wa makubaliano ya kuimarisha ushirikiano wa kiusalama kati ya nchi hizi mbili.' Hatua hii ya Washington, ambayo inafanyika kwa kisingizio cha "kuimarisha ushirikiano wa usalama na mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi ya Boko Haram na ISIS huko Afrika Magharibi", ni utambuzi wa kwanza rasmi wa uwepo wa moja kwa moja wa kijeshi wa Marekani katika nchi hii ya Kiafrika.
Katika miaka ya hivi karibuni, uwepo wa jeshi la Marekani barani Afrika hususan katika nchi za magharibi mwa bara hilo limekuwa suala zito. Uwepo huu, ambao awali uliambatana na visingizio kama vile kupambana na ugaidi na kuimarisha ushirikiano wa usalama, sasa umekuwa sehemu muhimu ya mkakati wa kimataifa wa Marekani. Licha ya madai kwamba madhumuni ya kutumwa kikosi hicho ni kupambana na makundi ya kigaidi kama vile Boko Haram na ISIS Afrika Magharibi, lakini ni wazi kuwa Marekani, katika kivuli cha kupambana na ugaidi, pamoja na masuala ya usalama, pia inafuatilia malengo ya kiuchumi na kijiopolitiki, ambayo kwa hakika yana mizizi katika tamaa ya nchi hii ya kupora rasilimali na utajiri wa Afrika. Kwa hivyo, Nigeria, kama nchi ambayo ina uchumi mkubwa zaidi katika bara la Afrika na rasilimali kubwa ya mafuta na gesi katika Ghuba ya Guinea, ni muhimu sana kwa Washington, haswa kwa vile kudhibiti rasilimali hizi kunamaanisha ufikiaji wa moja ya vituo vikuu vya nishati ulimwenguni.
Kwa upande mwingine, eneo la kimkakati la Nigeria huko Afŕika Maghaŕibi limeifanya kuwa lango la kupenya na kuingia katika nchi nyingine katika eneo hilo. Uwepo huu wa kijeshi unaunda kiungo kipya katika mlolongo wa muda mrefu wa uingiliaji wa Washington katika bara la Afrika na ni kisingizio cha kupanua kimya kimya na hatua kwa hatua duru ya ushawishi wa kijeshi wa Marekani katika maeneo ya kistratijia ya dunia, hususan miongoni mwa nchi zinazoizunguka Nigeria.
Hata hivyo, ukweli ni kwamba makundi ya kigaidi kama Boko Haram ni matokeo ya hali ngumu ya kijamii na kiuchumi katika nchi na eneo hilo. Kuenea kwa umaskini, ukosefu mkubwa wa ajira kwa vijana, rushwa, ubaguzi wa kikabila na kidini na utawala dhaifu ni mambo ambayo yamechangia katika kukua kwa makundi hayo na harakati za kigaidi nchini Nigeria na nchi nyingine jirani. Aidha baadhi ya makundi hayo ya kigaidi hupokea msaada wa kifedha kutoka kwa baadhi ya nchi za Magharibi. Uzoefu wa kihistoria umethisha kwamba uingiliaji wa kijeshi wa kigeni hauwezi kutoa suluhisho la kudumu kwa migogoro ya kijamii na kisiasa.
Mfano wazi wa kushindwa huku unaweza kuonekana wazi nchini Somalia. Tangu miaka ya 2000, Marekani imekuwa ikidai kwamba imeingia kwenye vita na al-Shabaab kwa kutumia mashambulizi ya ndege zisizo na rubani, kutuma washauri na kufanya operesheni maalum, lakini kundi hilo sio tu halijasambaratishwa, bali limeimarisha nguvu na kuendeleza mashambulizi yake katika nchi hiyo na katika nchi nyingine kadhaa jirani. Mfano mwingine ni Mali. Licha ya uwepo wa kijeshi wa miaka mingi wa Ufaransa kwa ushirikiano wa Marekani na kisha vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa, makundi ya kigaidi sio tu kwamba hayajarudi nyuma, bali yamepanua uwepo wao katika nchi jirani kama vile Burkina Faso na Niger, na hivyo wenyewe kuwa sababu ya ukosefu wa usalama katika eneo hilo.
Paul Pilar, mchambuzi mkuu wa zamani wa Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani kuhusu Masuala ya Afrika anaandika katika muktadha huu kwamba: "Mkakati wa Marekani katika pwani ya Afrika unategemea sana zana za kijeshi, mbinu ambayo inapuuza sababu za kisiasa na kiuchumi za kutokuwepo utulivu, na kwa hivyo haiwezi kudhamini usalama wa muda mrefu."
Mwishowe, inaonekana kwamba kutumwa kwa vikosi vya kijeshi vya Marekani nchini Nigeria ni hatua ya kimaonyesho tu ya kiusalama ambayo inafuatilia malengo ya kimkakati ya Washington katika kushindana na washindani wake wa kimataifa na kudumisha uwepo wake barani Afrika badala ya kushughulikia chanzo halisi cha migogoro. Kuhusiana na hilo, inaonekana kuwa njia bora zaidi ya kupambana na makundi ya kigaidi katika eneo hili ni kufikia suluhu ya ndani na ya pande zote kwa usihirikiano wa nchi za eneo sambamba na kukata uungaji mkono na misaada fiche ya kifedha kwa makundi hayo. Uwepo wa nguvu yoyote ya kigeni unazidisha tu matatizo ya eneo hilo na si vinginevyo.