Wasomi na wanafikra duniani watangaza kumuunga mkono Ayatullah Khamenei
https://parstoday.ir/sw/news/world-i136266-wasomi_na_wanafikra_duniani_watangaza_kumuunga_mkono_ayatullah_khamenei
Kundi la wasomi, wanafalsafa na wanaharakati kutoka sehemu mbalimbali za dunia limetangaza kumuunga mkono Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, pamoja na juhudi zake za ujasiri na zenye upeo mpana katika kulinda utu wa binadamu na haki.
(last modified 2026-02-05T02:35:37+00:00 )
Feb 05, 2026 02:35 UTC
  • Wasomi na wanafikra duniani watangaza kumuunga mkono Ayatullah Khamenei

Kundi la wasomi, wanafalsafa na wanaharakati kutoka sehemu mbalimbali za dunia limetangaza kumuunga mkono Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, pamoja na juhudi zake za ujasiri na zenye upeo mpana katika kulinda utu wa binadamu na haki.

Tamko hilo limetolewa kupitia taarifa iliyotiwa saini na watu mashuhuri na mashirika 46 kutoka mataifa na tamaduni tofauti.

Kwa mujibu wa ripoti ya Jumanne ya Shirika la Habari la Fars, katika taarifa hiyo, Ayatullah Khamenei alielezwa kuwa ni “kiongozi ambaye ushawishi wake unavuka mipaka ya kidini na kisiasa katika maendeleo ya fikra na maadili ya zama hizi.”

Waliotia saini, wakijitambulisha kama “wafuasi wa dini mbalimbali na watu huru wa dunia,” walisema wanampongeza Ayatullah Khamenei si kwa misingi ya dini pekee, bali kwa “msimamo wake thabiti juu ya maadili, ujasiri katika kufanya maamuzi, na maono ya kiustaarabu kuhusu mustakabali wa wanadamu.”

Waliongeza kuwa Ayatullah Khamenei ametekeleza sera na misimamo inayotetea haki ya mataifa, ikiwemo ya nchi yake, Iran, kujichagulia hatima yao wenyewe, licha ya gharama zinazohusiana na msimamo huo, hasa katika zama ambazo viongozi wengi wa dunia wamelegea mbele ya mashinikizo ya nguvu tawala.

Sehemu ya taarifa hiyo inasomeka hivi:  “Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni miongoni mwa viongozi wanaosimamia kwa uthabiti utu wa binadamu, uhuru wa kitaifa, haki, na msimamo wa kupinga dhuluma na utawala kiimla, katika dunia inayokumbwa na unafiki  na siasa zinazobadilika-badilika."

Wasomi na wanafikra hao, akiwemo mwanafalsafa wa Russia Aleksandr Dugin na mwandishi mashuhuri wa India Tushar Gandhi, walisema kuwa mfano wa uongozi wa Ayatullah Khamenei umejengwa juu ya misingi ya kibinadamu na wajibu wa kihistoria, hali inayochangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha mjadala wa kupinga dhuluma na ubeberu wa kimataifa.

Tamko hilo linakuja wakati ambapo vitisho vya kuibuka kwa vita vya Marekani dhidi ya Iran na uongozi wake wa kisiasa na kijeshi vinaongezeka.

Maafisa wa Iran wameonya kuwa watajibu kwa nguvu kubwa hatua yoyote ya kijeshi itakayochukuliwa dhidi ya nchi hiyo.

Aidha, onyo kutoka ndani na nje ya Iran limeeleza kuwa jaribio lolote dhidi ya maisha ya Ayatullah Khamenei litaibua ghadhabu kubwa katika eneo zima na ulimwengu mpana wa Waislamu.