Human Rights Watch: Israel inafanya mauaji ya halaiki Ukanda wa Gaza
-
Human Rights Watch: Israel inafanya mauaji ya halaiki Ukanda wa Gaza
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limetangaza kuwa, utawala wa Israel unafanya mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza, Palestina.
Philippe Bolopion, mkurugenzi mtendaji wa Human Rights Watch, amewashutumu wanajeshi wa utawala wa Kizayuni kwa kufanya mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza, akisema kwamba, shirika hilo limerekodi uhalifu mwingi uliofanywa na utawala wa Israel dhidi ya raia.
Philippe Bolopion amesema hayo katika mahojiano na kanali ya Televisheni ya al-Jazeera na kubainisha kwamba, serikali ya Marekani imeshindwa kuchukua hatua kali za kukomesha ukatili huko Gaza. Pia alisisitiza kwamba vurugu za walowezi katika Ukingo wa Magharibi zimefikia kilele, na kusababisha watu kuhama makazi yao.
Katika tukio linalohusiana na hilo, Human Rights Watch ilitangaza hapo awali kwamba, utawala wa Kizayuni umezuia haki ya wakimbizi wa Kipalestina kurudi katika ardhi zao.
Shirika hilo lilisisitiza kwamba mwenendo wa kufukuzwa Wapalestina bado unaendelea, likiona vitendo hivi kama uhalifu dhidi ya ubinadamu uliofanywa na utawala huo wa kibaguzi.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, mashambulizi mapya ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel yamewaua shahidi watu wasiopungua 20, wakiwemo watoto wadogo katika Ukanda wa Gaza.
Haya yanajiri siku chache baada ya Wapalestina wengine 31, wakiwemo watoto sita, kuuawa shahidi katika mashambulizi ya kinyama yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika Jiji la Gaza na mji wa Khan Younis katika Ukanda wa Gaza.
Wapalestina karibu 600 wameuliwa shahidi na jeshi la utawala wa Kizayuni tangu usitishaji mapigano uliosimamiwa na Marekani huko Gaza ulipoanza kutekelezwa Oktoba 10, 2025.