Rais wa Uturuki akosoa vikali hatua ya Israel ya kuitambua Somaliland
-
Rais wa Uturuki akosoa vikali hatua ya Israel ya kuitambua Somaliland
Rais Recep Tayyip Erdogani wa Uturuki amekosoa vikali hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kupuuza mamlaka ya kujitawala Somalia kwa kutambua jimbo lililojitenga na Somalia la Somaliland kama nchi huru.
Rais wa Uturuki amesisitiza kuwa, hatua hiyo ya Israel inakiuka uhuuru, mamlaka na umoja wa ardhi ya Somalia.
Rais Erdogan ameeleza kwamba, maamuzi kuhusu eneo la Somaliland yanapaswa kuzingatia "irada ya watu wote wa Somalia.
Hatua ya utawala ghasibu wa Israeli ya kutambua jimbo lililojitenga na Somalia la Somaliland kama nchi huru imeendelea kukosolewa na kulaaniwa kimataifa.
Aidha jumuiya mbalimbali za kieneo kama EAC, Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC na mataifa ya kikanda yameungana na walimwengu kupinga vikali hatua hiyo ya Israel yakisisitiza imekiuka kanuni na sharia za kimataifa.
Kwa upande wake Somalia imeendelea kupinga vikali kile ilichoeleza kuwa ni hatua isiyo halali ya Israel kutambua eneo lake lililojitenga la Somaliland, kama taifa huru. Serikali ya Mogadishu imetaja uamuzi huo kuwa ni uvunjaji wa mamlaka na umoja wa ardhi ya taifa.
Somalia imelaani hatua hiyo na kuitaja kuwa kitendo cha "uchokozi ambacho kamwe hakitavumiliwa.
Somaliland ilijitenga na Somalia mwaka 1991 kufuatia vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe lakini haijawahi kutambuliwa rasmi na nchi yoyote mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Jamhuri hiyo iliyotangaza kujitenga na Somalia imeanzisha sarafu yake, bendera na bunge, ingawa maeneo yake ya mashariki yameathiriwa na mzozo.