OCHA: DRC inakabiliwa na tishio la mgogoro mkubwa wa kibinadamu
-
OCHA: DRC inakabiliwa na tishio la mgogoro mkubwa wa kibinadamu
Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imeonya kuhusiana na mgogoro wa kutisha wa kibinadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Ripoti ya OCHA inaeleza kuwa, hali ya kibinadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imefikia viwango vikubwa.
Ripoti ya hivi karibuni ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA) inaeleza kuwa, nchi hiyo ilikuwa na zaidi ya watu milioni 5.3 waliokimbia makazi yao na karibu watu milioni 25 waliokabiliwa na uhaba wa chakula kufikia mwisho wa mwaka jana (2025). Takwimu hizi zinaonyesha mgogoro wa pande nyingi unaozidi kuwa mbaya kote nchini humo.
Tathmini ya kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi mwezi Desemba 2025 ni mbaya. Mbali na watu wengi kuhama makazi yao, OCHA imerekodi matukio 260,500 ya ulinzi, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, ukatili wa kijinsia, na mashambulizi kimwili kwa raia.
Uhaba wa chakula sasa unaathiri watu milioni 24.8. Kulingana na wataalamu wa masuala ya kibinadamu, kiwango hiki muhimu kinamaanisha kwamba karibu robo ya idadi ya watu wanajitahidi kukidhi mahitaji yao ya msingi ya lishe.
Ingawa mgogoro huu unaathiri sehemu za kati na magharibi mwa nchi, mikoa ya mashariki inaendelea kuwa mikoa iliyoathiriwa zaidi na kuhama kwa watu. Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, Ituri, na Tanganyika ni mikoa ambayo ina idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani milioni 5.3 waliohama makazi yao.
"Kaya zilizo katika mazingira magumu zaidi, hasa wanawake, watoto, na wazee, ndio waathiriwa wa kwanza wa mgogoro huu unaoongezeka," inabaainisa ripoti ya OCHA.