Iran yazindua miradi mitatu ya kimkakati ya teknolojia ya anga za mbali
Iran imezindua rasmi mafanikio matatu ya kimkakati ya ndani ya nchi katika sekta za miundombinu ya anga, mawasiliano na picha za satelaiti katika kuadhimisha Siku ya Kitaifa ya Teknolojia ya Anga za Mbali
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Iran, Sattar Hashemi, pamoja na Waziri wa Ulinzi, Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh, walihudhuria hafla hiyo iliyofanyika Jumanne katika mji mkuu, Tehran.
Katika hafla hiyo, mfano wa kwanza (prototype) wa kwanza wa mradi wa mfumo wa satelaiti uliopewa jina la aliyekuwa kamanda mashuhuri wa mapambano dhidi ya ugaidi, Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, umezinduliwa. Aidha, picha za kwanza zilizopigwa na setilaiti ya Paya ya Iran iliyotumwa hivi karibuni katika anga za mbali, zilionyeshwa, sambamba na kuzinduliwa kwa kituo kipya cha anga.
Kituo cha Anga cha Salmas, ambacho ni miongoni mwa miundombinu muhimu ya anga nchini , kilizinduliwa rasmi kaskazini-magharibi mwa Iran. Kituo hiki ni miongoni mwa vituo vikuu vya uendeshaji wa satelaiti, usimamizi wa misheni za anga, pamoja na upokeaji wa data na picha za satelaiti.
Kituo hicho kina miundombinu ya mawasiliano ya kisasa, mifumo ya usambazaji wa nishati, pamoja na vifaa vya kudhibiti misheni za setilaiti.
Kwa mujibu wa wataalamu wa teknolojia ya anga, nafasi ya kijiografia ya Kituo cha Anga cha Salmas hukiruhusu kufuatilia mizunguko ya satelaiti katika maeneo ya magharibi mwa nchi, na hata kufikia mamia ya kilomita zaidi ya mipaka ya taifa.
Uzinduzi wa kituo hiki umeongeza muda wa upatikanaji wa data za satelaiti na uwezo wa kutuma amri kwa satelaiti. Hatua hii ina mchango mkubwa katika kuongeza ufanisi wa misheni za anga za mbali, jambo muhimu sana katika enzi ya sasa ya teknolojia na uchumi wa kidijitali.
Katika hafla hiyo, pia mfano wa kwanza (prototype) wa mkusanyiko wa setilaiti wa Shahidi Soleimani ulizinduliwa, ukiwa na vipimo na sifa zake halisi na asilia.
Mfumo huo umebuniwa na kuendelezwa kikamilifu na wataalamu wa Iran, na unajumuisha takribani satelaiti 24. Umeundwa mahsusi kwa ajili ya kuwezesha mawasiliano ya masafa finyu (narrow-band) kwa eneo pana.
Kwa mujibu wa Shirika la Anga za Mbali la Iran, mkusanyiko wa satelaiti wa Shahidi Soleimani utawekwa katika mzunguko wa chini wa Dunia (Low Earth Orbit – LEO).
Mfumo huu unaweza kutumika kusafirisha data ndogo kwa ufanisi katika mazingira au hali nyeti, na pia kubadilishana data za vihisishi (sensor data) kwa lengo la kuendeleza huduma za Mtandao wa Vitu (Internet of Things – IoT) katika anga za mbali.
Katika sehemu nyingine ya hafla hiyo, picha za kwanza zilizopigwa na satelaiti ya hivi karibuni ya Iran iliyorushwa katika anga za mbali ijulikanayo kama Paya pia zilionyeshwa kwa hadhirina.
Satelaiti ya Paya inasemekana kuwa satelaiti nzito zaidi iliyoundwa Iran hadi sasa, ikiwa na uzito wa kilogramu 150, na kuashiria daraja jipya la teknolojia ya satelaiti ya Iran.
Paya inatumia teknolojia ya kamera ya kisasa yenye uwezo wa picha za msingi wa mita 5 kwa kila pikseli, ambao unaweza kuboreshwa hadi takriban mita 3 kwa kutumia algoriti za akili mnemba zilizoko ndani ya setilaiti.