Utafiti: Pombe, Sigara vinachangia ongezeko la ugonjwa wa saratani Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i136292-utafiti_pombe_sigara_vinachangia_ongezeko_la_ugonjwa_wa_saratani_kenya
Shirika la habari za afya la Willow limetangaza kuuwa, vidonda vya tumbo, uvutaji wa sigara, na matumizi ya pombe vinachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa ugonjwa wa saratani nchini Kenya.
(last modified 2026-02-05T14:02:51+00:00 )
Feb 05, 2026 12:47 UTC
  • Utafiti: Pombe, Sigara vinachangia ongezeko la ugonjwa wa saratani Kenya
    Utafiti: Pombe, Sigara vinachangia ongezeko la ugonjwa wa saratani Kenya

Shirika la habari za afya la Willow limetangaza kuuwa, vidonda vya tumbo, uvutaji wa sigara, na matumizi ya pombe vinachangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa ugonjwa wa saratani nchini Kenya.

Takriban watu 102,152 wamekuwa wakiishi na ugonjwa wa saratani nchini Kenya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Takwimu mpya za kimataifa zinaonyesha kuwa, kesi nyingi zinazohusiana na Helicobacter pylori (H. pylori), maambukizi ya Human Papillomavirus (HPV), na matumizi ya tumbaku zinaweza kuzuilika. Hayo ni kwa mujibu wa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).

Uchambuzi wa kimataifa uliofanywa na Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani (IARC), uliopewa jina Global and Regional Cancer Burden Attributable to Modifiable Risk Factors to Inform Prevention, umebaini kuwa karibu visa vinne kati ya kumi vya saratani duniani zinatokana na sababu zinazoweza kuzuilika. Hali hii inahusisha Kenya, ambapo saratani za tumbo, shingo ya kizazi, na mapafu bado ndizo zinazochangia zaidi kwa maradhi na vifo.

“Uchambuzi huu ni wa kwanza kuonyesha ni kiasi gani cha hatari ya saratani kinatokana na sababu tunazoweza kuzizuia,” alisema Dk. Andrew Ilbawi, Kiongozi wa Timu ya Udhibiti wa Saratani wa WHO na mwandishi wa utafiti. “Kwa kuchunguza mifumo ya nchi na makundi ya watu, tunaweza kuwapa serikali na wananchi taarifa za kina zaidi, zinazoweza kusaidia kuzuia visa vingi vya saratani kabla havijaanza.”

'Mwaka wa 2022 pekee, takriban kesi milioni 7.1 kati ya visa vipya vya saratani milioni 18.7 vilivyogunduliwa kati ya watu wazima vilichangiwa na sababu hizi 30 za hatari ambazo tulichunguza," Dk Isabelle Soerjomataram, Naibu Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi wa Saratani ya IARC na mwandishi mkuu wa utafiti huo.

Kwa kufafanua takwimu hizo zaidi, uvutaji sigara ulichangia takriban visa milioni 3.3 duniani kote, maambukizi kwa visa milioni 2.2 na pombe kwa takriban visa 700,000.