Tanzania yatoa tahadhari ya kuongezeka maambukizi ya mafua, Covid 19 na Dengue
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i137038-tanzania_yatoa_tahadhari_ya_kuongezeka_maambukizi_ya_mafua_covid_19_na_dengue
Wizara ya Afya ya Tanzania imetoa tahadhari ya afya kwa umma ya kuongezeka kwa maambukizi ya mafua na Uviko-19 na kuongezeka kwa hatari ya homa ya dengue, huku ikiwataka wananchi kuchukua hatua za haraka za kujikinga hasa katika kipindi cha msimu wa mvua.
(last modified 2026-02-26T03:44:23+00:00 )
Feb 26, 2026 03:44 UTC
  • Tanzania yatoa tahadhari ya kuongezeka maambukizi ya mafua, Covid 19 na Dengue

Wizara ya Afya ya Tanzania imetoa tahadhari ya afya kwa umma ya kuongezeka kwa maambukizi ya mafua na Uviko-19 na kuongezeka kwa hatari ya homa ya dengue, huku ikiwataka wananchi kuchukua hatua za haraka za kujikinga hasa katika kipindi cha msimu wa mvua.

Katika taarifa hiyo Jumatano, Wizara ilisema taarifa za uchunguzi kutoka vituo vya afya zinaonyesha idadi inayoongezeka ya wagonjwa wanaoonyesha dalili za matatizo ya mfumo wa kupumua ikiwa ni pamoja na homa, kikohozi, koo, mwili kudhoofika na tatizo la upumuaji, - ishara zinazohusiana na mafua na Uviko -19.

‘‘Upimaji wa kimaabara umethibitisha kuendelea kusambaa kwa virusi hivyo, lakini tunauhakikishia umma kuwa maambukizi mengi ni hafifu na wagonjwa wanapona", alisema Dkt Grace Magembe Mganga Mkuu wa serikali.

Wizara ilisema hali bado inadhibitiwa na inafuatiliwa kwa karibu kupitia mfumo wa kitaifa wa ufuatiliaji wa magonjwa, huku vituo vya afya vikielekezwa kuhakikisha upatikanaji wa dawa muhimu, oksijeni na huduma za upimaji na kuripoti mara moja maambukizi yanayoshukiwa.

Sambamba na maambukizi ya njia ya kupumua, serikali pia ilionya kuhusu hatari kubwa ya homa ya dengue kutokana na mvua zinazoendelea zinazochangia mazingira ya mbu kuzaliana.

Wananchi wametakiwa kuondoa maji yaliyotuama majumbani, kutupa ipasavyo vyombo vinavyoweza kukusanya maji ya mvua, kufyeka vichaka, kutumia dawa za kuua mbu na kutafuta huduma ya matibabu mapema pale dalili zinapoonekana.

Mkazo maalum uliwekwa katika kulinda vikundi vilivyo katika hatari kubwa ikiwa ni pamoja na wazee, wanawake wajawazito na watu binafsi wenye magonjwa sugu.../