Jibu la kulipiza kisasi la Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni lilitolewa kwa msingi wa sheria za kimataifa
(last modified Sun, 06 Oct 2024 02:23:59 GMT )
Oct 06, 2024 02:23 UTC
  • Jibu la kulipiza kisasi la Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni lilitolewa kwa msingi wa sheria za kimataifa

Licha ya kuwa jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limetekeleza Operesheni ya "Ahadi ya Kweli 2" kwa ajili ya kuonyesha uwezo wake wa kistratijia wa kuuadhibu utawala wa Kizayuni wa Israel, lakini wakati huo huo ni wazi kuwa hatua hiyo iliyochukuliwa kwa ajili ya kulinda heshima ya taifa la Iran imefanyika kwa msingi wa sheria za kimataifa.

Vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya kujizuia kwa muda kuchukua hatua za kukabiliana na ukiukwaji wa mamlaka na ardhi yake na vitendo vya jinai vya utawala wa Kizayuni katika kuwaua kigaidi Masdhahidi Ismail Haniyeh, Seyed Hassan Nasrallah, Meja Jenerali Seyed Abbas Nilfroushan na mauaji ya kimbari dhidi ya wanawake na watoto wasio na hatia huko Palestina na Lebanon, mnamo Oktoba 1, vilitekeleza operesheni ya "Ahadi ya Kweli II", kwa kuvurumisha mamia ya makombora ya balestiki kuelekea vituo vya kiusalama, kijeshi na kijasusi vya utawala wa Kizayuni. Haua hiyo ilichukuliwa kwa msingi wa sheria inayozipa nchi haki ya kujilinda dhidi ya uchokozi wa adui kwa mujibu wa kifungu cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa,

Makombora ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC yalilenga kwa mafanikio vituo vya kiusalama na kijasusi vya utawala wa Kizayuni katika Operesheni ya "Ahadi ya Kweli II" kwa kauli mbiu tukufu ya "Ya Rasulullah", ambapo asilimia 90 ya makombora hayo yalifanikiwa kufika na kuharibu maeneo yaliyolengwa. Kufuatia mafanikio hayo utawala wa Kizayuni uliingiwa na wasi wasi na kupatwa na kiwewe kikubwa kuhusu namna Iran ilivyoweza kufanikiwa kupata habari na siri na kiusalama za maeneo hayo yanayopewa ulinzi mkali kupindukia. Operesheni hii ilitekelezwa kwa idhini ya Baraza Kuu la Usalama la Taifa na kupewa taarifa Kamandi Kuu ya Majeshi ya Iran na kwa uungaji mkono wa Jeshi la kawaida la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Wizara ya Ulinzi.

Baada ya kutekelezwa operesheni hiyo viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamekuwa wakisisitiza kuwa, operesheni hiyo imefanyika kwa ajili ya kukabiliana na jinai na shari za mara kwa mara za utawala wa Kizayuni katika eneo, na kwamba Iran daima iko tayari kuchukua hatua zaidi za kuuadhibu iwapo utaendelea kuibua migogoro dhidi ya mataifa ya eneo hili. Wanasisitiza kuwa jeshi la Iran liko tayari wakati wowote kutoa jibu linalonasibiana na jinai na chokochoko zinazoibuliwa na utawala huo.

Operesheni ya "Ahadi ya Kweli II" imethibitisha wazi kuwa Iran inao uwezo wa kutosha wa kijeshi kwa ajili ya kuleta uthabiti na usalama katika eneo na kukabiliana vilivyo na chokochoko za mara kwa mara za Wazayuni, chokochoko ambazo bila shaka zinatekelezwa kwa uungaji mkono kamili wa kijeshi na kifedha wa nchi za Magharibi. Kama tulivyotangulia kusema operesheni hii imetekelezwa kwa kuzingatia sheria za kimataifa na kwa mujibu wa kifungu cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa, ambacho kinaipa kila nchi haki ya kujilinda dhidi ya maadui.

Operesheni ya "Ahadi ya Kweli 2"

Hoja kuu inayotegemewa na Iran katika kutoa jibu kali dhidi ya uchokozi wa utawala wa Kizayuni, ni kifungu cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa, ambacho kinaziruhusu nchi zote kukabiliana na kumuadhibu mchokozi katika fremu ya haki ya asili ya kutetea utawala na ardhi zao dhidi ya vitisho na hujuma kutoka nje. Kulinda nchi dhidi ya mashambulizi ya kijeshi au ya kigaidi inatambuliwa kuwa sehemu muhimu ya mfumo wa sheria za kimataifa.

Akihutubia umati mkubwa wa waumini waliokusanyika katika Muswala wa Imam Khomeini kwa ajili ya kutekeleza wajibu muhimu wa kiibada na kisiasa wa Swala ya Ijumaa, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema kuwa umoja na mshikamano kati ya Waislamu huwaletea rehema, heshima na ushindi dhidi ya maadui kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kusisitiza kuwa: "Kwa msingi wa sheria za kujilinda za Uislamu, katiba ya Jamhuri ya Kiislamu na sheria za kimataifa, kazi nzuri ya jeshi ilikuwa hatua ya kisheria na halali. Ni adhabu ndogo tu ambayo amepewa Mzayuni mtendajinai na mfyonzadamu. Jamhuri ya Kiislamu itatekeleza majukumu yake kwa ujasiri na azma thabiti. Hatutasita, kufanya mambo kwa pupa wala kuzembea katika kumuadhibu mchokozi."

Operesheni ya "Ahadi ya Kweli 2" ni hatua ya kistratijia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo imetekelezwa kwa ajili ya kulinda uthabiti na usalama wa eneo, usalama ambao umevurugwa na kifikia kilele cha ghasia kutokana na siasa za kuibua mivutano na migogoro za utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wake wa Magharibi. Kutetea wanyonge na kutegemea uwezo wa ndani pia ni ujumbe mwingine muhimu wa operesheni hii kwa nchi rafiki za Iran na eneo zima la Asia Magharibi.