Trump na Netanyahu wajadili kuwahamisha Wapalestina kwa nguvu Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i128092-trump_na_netanyahu_wajadili_kuwahamisha_wapalestina_kwa_nguvu_ghaza
Waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu amekutana na Rais wa Marekani Donald Trump katika Ikulu ya White House, huku viongozi hao wawili wakirudia pendekezo lao tata la kuwahamisha kwa nguvu maelfu ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.
(last modified 2025-07-08T23:08:12+00:00 )
Jul 08, 2025 12:29 UTC
  • Trump na Netanyahu wajadili kuwahamisha Wapalestina kwa nguvu Ghaza

Waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu amekutana na Rais wa Marekani Donald Trump katika Ikulu ya White House, huku viongozi hao wawili wakirudia pendekezo lao tata la kuwahamisha kwa nguvu maelfu ya Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza.

Trump na Netanyahu walikutana kwa chakula cha jioni katika chumba cha Blue Room cha White House siku ya Jumatatu huku mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yakiwa yanafanyika nchini Qatar kati ya Israel na harakati ya Hamas kujadili mapendekezo yanayoungwa mkono na Marekani ya kusitisha mapigano kwa siku 60 ili kuhitimisha vita vya Ghaza vilivyodumu kwa miezi 22 yakionekana kushika kasi.

"Tunashirikiana na Marekani kwa karibu sana kuhusiana na kutafuta nchi ambazo zinataka kutimiza kile zinachosema kila mara, kwamba zinataka kuwapatia Wapalestina maisha bora ya baadaye. Nadhani tunakaribia kupata nchi kadhaa."

Wataalamu mbali mbali wakiwemo wa masuala ya sheria wanasema, hilo ni jambo ambalo viongozi wa utawala ghasibu wa kizayuni wamekuwa wakilizungumzia kwa muda sasa, wakiliita 'uhamaji wa hiari' wa Wapalestina katika ardhi yao huku likilaaniwa kwa kutambuliwa kuwa ni hatua ya ufutaji wa kizazi.

Trump na Netanyahu wamekutana wakati wawakilishi wa Israel na Hamas wanaendelea na mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kwa siku ya pili nchini Qatar.

Ikiwa mapatano yatafikiwa, mpango wa kusitisha mapigano kwa siku 60 utashuhudia kuachiliwa kwa awamu kwa mateka wa kizayuni wanaoshikiliwa na Hamas na wafungwa wa Kipalestina wanaosota kwenye magereza ya utawala wa kizayuni, kuondoka wanajeshi wa Israel maeneo ya Ghaza, na majadiliano juu ya kukomesha vita kikamilifu…/