Euro-Med: Trump afunguliwe mashitaka kwa mauaji ya Wapalestina wanaotafuta misaada
https://parstoday.ir/sw/news/world-i128282
Kituo cha Euro-Mediterranean Human Rights Monitor kimeikashifu taasisi ya Gaza Humanitarian Foundation (GHF), inayofadhiliwa na Marekani pamoka na utawala haramu wa Israel, kwa mashambulizi ya mara kwa mara na yenye umwagaji damu dhidi ya raia wenye njaa wanaokusanyika kupokea misaada katika Ukanda wa Gaza, kikitoa wito wa kusitishwa haraka shughuli zote za GHF.
(last modified 2025-07-13T14:06:14+00:00 )
Jul 13, 2025 14:06 UTC
  • Euro-Med: Trump afunguliwe mashitaka kwa mauaji ya Wapalestina wanaotafuta misaada

Kituo cha Euro-Mediterranean Human Rights Monitor kimeikashifu taasisi ya Gaza Humanitarian Foundation (GHF), inayofadhiliwa na Marekani pamoka na utawala haramu wa Israel, kwa mashambulizi ya mara kwa mara na yenye umwagaji damu dhidi ya raia wenye njaa wanaokusanyika kupokea misaada katika Ukanda wa Gaza, kikitoa wito wa kusitishwa haraka shughuli zote za GHF.

Shirika hilo la haki za binadamu lenye makao yake mjini Geneva, katika ripoti iliyotolewa Jumamosi, limeitaka jumuiya ya kimataifa kuanzisha uchunguzi wa kina kuhusu taarifa za uhalifu wa kivita.

Ripoti hiyo imeangazia tukio la hivi karibuni la mauaji katika eneo la ash-Shakoush, Rafah, ambapo Wapalestina 30 waliuawa na zaidi ya wengine 180 kujeruhiwa vibaya.

Tukio hilo lilitokea baada ya kufungwa kwa vituo vya misaada, hali iliyowalazimu maelfu ya watu kukusanyika kwa wingi katika eneo moja, katikati ya mzingiro wa kinyama unaotekelezwa na Israel.

Mashuhuda na video zilizopitiwa na Euro-Med zinaonesha kuwa walinzi binafsi wa usalama kutoka Marekani, kwa kushirikiana na wanajeshi wa Israel, walifyatua risasi  na gesi ya kutoa machozi dhidi ya raia waliokuwa wakitafuta chakula.

Euro-Med Monitor imeishtaki GHF kwa kugeuza misaada ya kibinadamu kuwa silaha ya njaa na vifo chini ya usimamizi wa jeshi la Israel, hali ambayo imepindua mfumo wa awali wa Umoja wa Mataifa wa usambazaji wa misaada.

Shirika hilo la haki za binadamu limetaka uwajibikaji wa kisheria dhidi ya wahusika wote, akiwemo Rais Donald Trump wa Marekani, kwa kuunga mkono mfumo wa misaada unaoongozwa na Israel na pia kwa msaada mkubwa wa kijeshi na kidiplomasia alioutoa kwa kampeni ya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza.

Trump na Netanyahu

Limeeleza kuwa matumizi ya nguvu zinazosababisha vifo vya raia katika maeneo ya misaada ni kinyume cha sheria za kimataifa, na ni jinai ya kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu na mauaji ya kimbari.

Euro-Med imeitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua, ikiwemo kuiwekea Israel vikwazo, kufungua tena njia za upatikanaji wa misaada kwa Gaza, na kuhakikisha wahusika wa uhalifu huo wanachukuliwa hatua za kisheria kupitia mahakama na mifumo ya kimataifa ya haki.

Mpalestina mmoja aliyenusurika katika mauaji hayo ameiambia timu ya Euro-Med jinsi raia waliokuwa wakijificha kwenye shimo karibu na eneo la misaada walivyoshambuliwa na vifaru na walenga shabaha wa mbali, matukio yaliyosababishia mauaji makubwa ndani ya saa moja.

Shirika hilo limeonya kuwa usimamizi wa misaada unaofanywa na GHF unaweka maisha ya Wapalestina katika hatari kubwa. Limependekeza kurejeshwa kwa usambazaji wa misaada chini ya uongozi huru wa Umoja wa Mataifa ili kuepuka mauaji zaidi katika Ukanda wa Gaza.

Takwimu zinaonesha kuwa watu wasiopungua 58,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa huku wengine 138,095 wakijeruhiwa tangu kuanza kwa mashambulizi makali ya Israel dhidi ya Gaza tarehe 7 Oktoba 2023.

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imeshatoa hati za kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na aliyekuwa waziri wa vita, Yoav Gallant, mwezi Novemba mwaka jana, kwa jinai za kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Aidha, Israel inakabiliwa na kesi ya mauaji ya kimbari katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kutokana na vita vyake dhidi ya Gaza, eneo linalozingirwa hadi leo.