Takwa na msisitizo wa Iran wa kuimarisha mtazamo wa eneo kuwa na mwelekeo wa pamoja katika sera za nje
Alireza Enayati, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Saudi Arabia amesema: Iran ina nia ya dhati ya kuimarisha ushirikiano wa pande mbili na wa pande kadhaa na kuimarisha mtazamo wa eneo kuwa na mwelekeo wa pamoja kwa ajili kufikia ustawi na kuwa na usalama halisi.
Suala la kuwa na muelekeo wa pamoja wa kikanda ni mojawapo ya stratejia muhimu zaidi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uga wa sera za nje. Ukweli ni kwamba, "Muelekeo wa Pamoja wa Kieneo" (Regionalism) ni moja ya misamiati inayokaririwa mara kwa mara katika uga wa sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambayo imekuwepo tangu huko nyuma na imepewa umuhimu zaidi katika miaka ya hivi karibuni.

Kuna sababu kadhaa zinazoifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ijikite na kutilia mkazo suala la muelekeo wa pamoja wa kikanda katika siasa zake za nje. Sababu ya kwanza ni kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kuwa usalama wa eneo hili unapaswa kudhaminiwa na nchi zenyewe za eneo; na kwamba nchi za kigeni, sio tu hazina uwezo wa kuhakikisha usalama wa eneo hili, bali ndizo zinazovuruga amani na usalama wake. Sababu nyingine ni kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kwamba, uwezo na fursa za eneo zinaweza kutumika kwa ajili ya maendeleo ya nchi na vilevile kwa maendeleo katika ngazi ya kieneo. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatilia mkazo kuwepo muelekeo wa pamoja katika nyanja mbalimbali kwenye ngazi ya kieneo. Kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, muelekeo wa pamoja wa kieneo si tu unawezesha kuwepo ushirikiano baina ya nchi za eneo, lakini wakati huo huo, unaifanya pia mikakati ya kihasimu ya maadui dhidi ya eneo hili na dhidi ya uhusiano kati ya nchi za eneo isiwe na taathira; na hivyo kuzifanya nchi hizo zichukue hatua ya kuzidishia kiwango cha ushirikiano wao na kustawisha mahusiano ya pande mbili baina yao.
Moja ya matokeo muhimu zaidi ya kuwepo muelekeo wa pamoja katika sera za kigeni ni kupatikana uwezekano wa kuongezwa pia kiwango cha miamala ya kiuchumi kati ya nchi husika. Wakati huo huo, mwelekeo wa pamoja wa kikanda huziwezesha nchi kuwa na uelewa wa pamoja wa vitisho na fursa zilizopo na kuchukua hatua za kivitendo za kupunguza vitisho vinavyozikabili. Mwelekeo wa pamoja wa kikanda sio suala linalohusiana na nchi zinazoendelea tu, lakini hata nchi zilizoendelea na za kiviwanda duniani nazo pia zimefuata katika siasa zao za nje, njia ya muekeleo wa pamoja wa kikanda; Umoja wa Ulaya ukiwa ni moja ya mifano hai ya suala hili.
Katika miaka ya hivi karibuni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imechukua hatua za kivitendo za kuimarisha muelekeo wa pamoja wa kieneo, ikiwa ni pamoja na kutekeleza mkakati wa kustawisha uhusiano na nchi jirani, suala ambalo lilipewa uzito na mazingatio maalumu na serikali iliyopita ya awamu ya 13 na kuendelezwa na serikali ya sasa ya awamu ya 14.

Katika miaka ya karibuni, na katika kuimarisha muelekeo wa pamoja wa kikanda, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejiunga na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai na Kundi la kiuchumi la BRICS; na hizi ni miongoni mwa ishara za azma na irada thabiti iliyonayo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuimarisha suala hilo. Kuhusiana na suala hilo, Alireza Enayati, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Riyadh amesisitiza katika kikao cha Jukwaa la Ushirikiano wa Asia (ACD) kilichofanyika huko Doha mji mkuu wa Qatar chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al Thani, ya kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nia ya dhati katika kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa pande mbili na wa pande kadhaa na kuimarisha suala la kuwa na mwelekeo wa pamoja ili kufikia ustawi na usalama halisi.