Oct 07, 2024 10:52 UTC
  • Emmanuel Macron
    Emmanuel Macron

Wito wa Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, wa kusitishwa msaada wa silaha kwa utawala bandia na ghasibu wa Israel umefuatiwa na jibu kali la Waziri Mkuu wa utawala huo, Benjamin Netanyahu.

Akizungumza na kituo cha redio ya Ufaransa, Macron amesema: "Kipaumbele cha sasa ni kurejea kwenye suluhisho la kisiasa na kuacha kutuma silaha ambazo zinatumika katika vita huko Gaza."

Wakati huu ambapo Wazayuni wanaendelea kuishambulia Lebanon kwa mabomu, usiku na mchana, Rais wa Ufaransa ameongeza kuwa: “Kipaumbele chetu hivi sasa ni kuepusha kuongezeka mivutano. Watu wa Lebanon hawapaswi kuwa wahanga; Lebanon haiwezi kuwa Gaza nyingine."

Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel amekasirishwa na ombi hilo la kipropaganda la Rais wa Ufaransa la kusimamisha upelekaji wa silaha kwa serikali ya Tel Aviv ambazo zinatumika katika mauaji ya kimbari akiyata kuwa "yanatia aibu"!

Macron na Netanyahu

Mara tu baada ya jibu la Netanyahu kwa matamshi hayo ya Macron, Ikulu ya Elysee imesema katika taarifa yake kwamba Macron "anaunga mkono na ameonyesha uungaji mkono wake kwa usalama wa Israel."

Matamshi hayo ya Macron yametolewa huku serikali ya Paris, pamoja na Marekani ambayo ni mshirika mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, ikiendelea kutoa himaya na misaada ya kidiplomasia na kisiasa kwa utawala huo katili kwa ajili ya kuendeleza jinai zake za kivita huko Gaza na kuua Wapalestina.

Hadi sasa, Ufaransa haijaunga mkono hatua za kisheria zilizochukuliwa na nchi nyingine dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu na Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu kuhusu tuhuma za kuhusika na mauaji ya kimbari huko Gaza. Hii ni licha ya kwamba, utawala huo umeendelea kukiuka sheria za kimataifa za vita na unashambulia maeneo ya kiraia, ikiwa ni pamoja na misikiti, makanisa, hospitali, vitongoji vya makazi ya watu, vituo vya elimu na taasisi za misaada za Umoja wa Mataifa. Asilimia 85 ya wakazi wa Gaza wameyakimbia makazi yao kutokana na vita na hawawezi kurejea kwenye makazi yao yaliyoharibiwa kikamili. Vilevile mashambulizi ya Israel yameharibu kabisa zaidi ya 60% ya miundombinu muhimu ya Gaza.

Licha ya uharibifu huo mkubwa na mashambulizi ya kikatili ya Wazayuni, hakuna mpango wa kivitendo uliobuniwa katika ngazi ya kimataifa wa kusimamisha vita na mauaji ya Israel. Kwa maneno mengine ni kuwa, sheria za kimataifa zinapuuzwa kwa urahisi katika maeneo ambayo hayahusiani au kugusa maslahi ya nchi za Magharibi. Katika mwaka uliopita, hakuna sheria ya kimataifa ambayo haikuvunjwa wana hakuna jinai na uhalifu ambao haujaifanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel. Kama Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anajaribu kuchukua nafasi ya mwanaharakati wa kukomesha uvamizi wa Wazayuni huko Lebanon, sio kwa sababu ya Wazayuni kukiuka sheria za kimataifa na kanuni za kibinadamu, la hasha, bali ni kwa sababu ya maslahi ya Wafaransa katika koloni la zamani la nchi hiyo eneo la Asia Magharibi. 

Emmanuel Macron

Naam, badala ya kujibu matusi na dharau ya Netanyahu aliyeponda matamshi na wito wake wa kusitishwa utumaji wa silaha huko Israel, Rais wa Ufaransa ametoa taarifa na kutangaza msimamo wake wa kuunga mkono kikamilifu utawala wa Kizayuni wa Israel. Ofisi ya Macron imesema: Ufaransa ni rafiki thabiti wa Israel. Katika mkondo huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot amepanga kutembelea Israel. 

Kwa sera hizi za kinafiki na za kuuma na kupuliza za Ufaransa, na himaya na misaasa ya serikali za nchi za Ulaya na Marekani, tusitarajie kuona harakati yoyote ya Macron na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa ikisimamisha tingatinga la mauaji ya kimbari ya Netanyahu kwa maslahi ya watu wa Palestina au Lebanon.