Feb 18, 2020 07:52 UTC
  • Spika wa Iran akutana na Rais wa Lebanon na Sayyid Nasrullah

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Michel Aoun wa Lebanon, Spika wa Bunge la nchi hiyo ya Kiarabu, Nabih Berri na Katibu Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrullah mjini Beirut.

Larijani amekutana kwa nyakati tofauti na Rais Aoun na Spika wa Bunge la Lebanon, ambapo wamejadili masuala yenye maslahi ya pande mbili, ikiwemo haja ya kuimarisha uhusiano wa Beirut na Tehran katika nyuga mbalimbali, pamoja na masuala ya kieneo.

Katika mazungumzo baina ya Sayyid Hassan Nasrullah na Spika wa Bunge la Iran, masuala ya kieneo na mbinu za kupatia ufumbuzi changamoto za kiusalama, kiuchumi kisiasa mingoni mwa nchi za kieneo ni katika ajenda za mkutano huo wa jana Jumatatu.

Dakta Larijani ameashiria pia uwezo wa Iran na Lebanon kwa ajili ya kupanua ushirikiano wao katika uga wa kiuchumi na kueleza bayana kwamba, Tehran iko tayari kuipatia tajiriba na uzoefu wake Beirut katika nyanja za kilimo na petrokemikali na kushiriki katika miradi ya pamoja.

Spika Larijani (kushoto) na Sayyid Nasrullah

Kabla ya kukutana na viongozi hao wa Lebanon, Dakta Ali Larijani, amezungumzia pia mpango wa Marekani-Kizayuni wa Muamala wa Karne na kusema kuwa, mpango huo umezaliwa hali ya kuwa umekufa hivyo hautakuwa na matunda yoyote.

Kabla ya kwenda Lebanon, Spika wa Bunge la Iran aliitembelea Syria na kufanya mazungumzo na Rais Bashar al-Assad pamoja na viongozi wengine wa ngazi za juu wa nchi hiyo ya Kiarabu, ambapo alisisitiza kuendelea uungaji mkono wa Tehran kwa Damascus katika vita dhidi ya magaidi.

Tags