Feb 13, 2026 02:24 UTC
  • Leo katika historia
    Leo katika historia

Leo ni Ijumaa 24 Sha'ban 1447 Hijria sawa na 13 Februari 2026.

Katika siku kama ya leo miaka 337 iliyopita tangazo lililojulikana kama Tangazo la Sheria lilisomwa katika sherehe za kumvika taji Mfalme William wa Tatu na Malkia Marry wa Pili wa Uingereza na kuanzia hapo mfumo wa utawala wa nchi hiyo ukabadilika na kuwa utawala wa kifalme wa kikatiba.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, madaraka ya Mfalme wa Uingereza yalipunguzwa na kukabidhiwa bunge la nchi hiyo.    ***

Siku kama ya leo miaka 135 iliyopita, alifariki dunia Mirza Muhammad Hassan Shirazi, mmoja wa wanazuoni na mar'ja' mashuhuri wa Kiislamu.  

Alizaliwa mwaka 1230 katika mji wa Shiraz kusini mwa Iran. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi alielekea katika mji mtakatifu wa Najaf nchini Iraq kuendeleza masomo yake ya kidini na kupata elimu kwa wanazuoni mashuhuri wa mji huo kama Sheikh Murtadha Ansari.

Jina la Mirza Shirazi ni mashuhuri mno kutokana na fatuwa ya kuharamisha tumbaku. Fatua yake hiyo ya kuharamisha tumbaku na matumizi ya sigara, bidhaa ambayo ilikuwa ikihodhiwa na Uingereza, ilitoa pigo kubwa kwa ukoloni wa Uingereza nchini Iran. Vilevile fatua hiyo ilitambuliwa kuwa mapambano ya moja kwa moja dhidi ya utawala wa Shah na ukoloni wa Uingreza nchini Iran na iliandaa uwanja wa mapambano ya baadaye ya wananchi wa Iran dhidi ya dhulma, ukandamizaji na ukoloni wa wageni.     ****

Siku kama ya leo mwaka 1946 wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, ndege za kivita za Uingereza na Marekani zilianza kudondosha zaidi ya tani 3900 za mabomu katika mji wa Dresden nchini Ujerumani.

Mashambulizi hayo yaliua zaidi ya watu 25,000 na kusababisha majonzi na vilio kote duniani.   ****

Miaka 38 iliyopita katika siku kama hii ya leo, aliaga dunia Ayatullah Sheikh Salman Khaqani.

Alizaliwa mwaka 1293 Hijria Shamsia katika moja ya miji ya kusini mwa Iraq ya leo. Baada ya kupitisha kipindi cha utoto, akiwa na umri wa miaka 13 alihajiri na kuelekea Najaf al-Ashraf nchini Iraq kwa ajili ya kusoma masomo ya dini. Akiendelea na masomo yake, Sheikh Salman Khaqani hakuacha kujihusisha na harakati za kijamii, kiasiasa na kifasihi. Akiwa na umri wa miaka 43 na baada ya kufariki dunia baba yake aliyekuwa mmoja wa maulama wa Khorramshahr kusini mwa Iran aliuchagua mji huo kuwa makazi yake.

Katika kipindi cha miongo mitatu ya kuishi kwake huko Khorramshahr, mwanazuoni huyo aliondokea kuwa chanzo cha uongofu wa watu na kufanikiwa kutoa huduma zenye thamani kubwa.

Baada ya kuanza vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa Baath wa Iraq, nyumba ya alimu huyo ilikuwa kimbilio la watu hadi nyumba hiyo iliposhambuliwa na kubomolewa kwa mabomu ya jeshi la Saddam Hussein.       *******