Uchunguzi wa matokeo ya mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Lebanon na Palestina
Utawala wa Kizayuni wa Israel unatumia silaha zilizopigwa marufuku kushambulia maeneo ya raia ya Lebanon na Ukanda wa Gaza.
Baada ya kuanza kwa Oparesheni Kimbunga cha Al-Aqsa, na mashambulizi ya jeshi la Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza, zilichapishwa ripoti kuhusu matumizi ya silaha za maangamizi umati huko Ukanda wa Gaza. Ripoti hizo zinaonyesha kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel pia umetumia mabomu yenye madini ya urani iliyohafifishwa katika mashambulizi yake ya hivi karibuni dhidi ya Lebanon. Kwa mujibu wa arifisho la kijeshi, mabomu yenye urani iliyohafifishwa hayatambuliwa kuwa ni silaha za nyuklia, lakini kutokana na madhara makubwa ya matumizi ya silaha hizo katika vita, hasa kwa ya watu wa kawaida, Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), limetahadharisha kuhusu hatari ya miali ya silaha hizo kwa raia.

Kundi la wanasayansi wa Lebanon limetahadharisha kuwa, kwa mujibu wa ushahidi uliopo, utawala wa Kizayuni umetumia mabomu yenye madini ya urani iliyohafifishwa kushambulia nchi hiyo. Jumuiya ya Wanakemia nchini Lebanon pia imelaani "mashambulizi ya kikatili" wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya raia wa nchi hiyo na kuonya kuhusu athari za kuvuta vumbi la hujuma hiyo ya mabomu.
Katika taarifa ya wanakemia wa Lebanon imeelezwa kuwa, kiwango cha uharibifu wa mabomu yaliyotumika katika majengo ambayo yamechimba makumi ya mita chini ya ardhi, kinaashiria matumizi ya mabomu yenye urani iliyohafifishwa, (depleted uranium) ambayo ina uwezo wa kupenya na kuingia ndani kabisa. Taarifa hiyo imesema: Utumiaji wa silaha hizo zilizopigwa marufuku kimataifa, hasa katika mji wenye msongamano mkubwa wa watu wa Beirut, unasababisha uharibifu mkubwa, na vumbi linalotokana na mashambulizi hayo pia, husababisha magonjwa mengi, hasa wakati wa kuvuta pumzi.
Utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukishambulia maghala ya vyakula na vyombo vya nyumbani kwa madai kuwa Hizbullah inatumia maghala hayo kuhifadhia silaha.

Katika mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni huko Ukanda wa Gaza kulichapishwa pia ripoti kwamba, Wazayuni wametumia silaha zilizopigwa marufuku. Utawala wa Kizayuni unatumia silaha hizo katika mauaji ya kimbari ya watu wasio na ulinzi licha ya kwamba, kwa mujibu wa sheria za kimataifa za vita, matumizi ya silaha hizo dhidi ya raia wa kawaida yanahesabiwa kuwa ni jinai ya kivita.
Baada ya kuanza Oparesheni ya Kimbunga ya Al-Aqsa, utawala wa Kizayuni umeshindwa kukabiliana na makundi ya Muqawama ya Palestina na Lebanon licha ya himaya na misaada ya pande zote ya kifedha na silaha ya Marekani na Magharibi kwa ujumla; hivyo umeamua kutumia jinai za aina zote kwa ajili ya kufikia malengo yake maovu na yasiyo ya kibinadamu. Kiwango kikubwa cha matumizi ya silaha zilizopigwa marufuku kinaonyesha kuwa, uhalifu huu wa kinyama wa utawala katili wa Israel usingewezekana bila msaada wa Marekani.

Kuendelea kwa vita huko Ukanda wa Gaza na Lebanon kumedhihirisha kuwa, utawala wa Kizayuni ndio chanzo kikuu cha kukiukwa sheria za kimataifa za vita. Mauaji ya kupangwa huko Ukanda wa Gaza na mashambulizi makubwa katika maeneo ya makazi ya watu nchini Lebanon ndiyo lengo kuu la jeshi la utawala wa Kizayuni; na Marekani na nchi za Magharibi ni washirika katika uhalifu huo unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel.
Jinai hizo za utawala wa Kizayuni, zinafanyika huku wanaodai kutetea haki za binadamu wakiwa wamenyamaza kimya mbele ya uhalifu huo' na licha ya maandamano yanayofanyika katika maeneo tofauti ya dunia dhidi ya Wazayuni na kuwatetea Wapalestina, maafisa wa nchi za Magharibi bado hawajaachana na mwenendo wao wa siku zote na wanaendelea kupeleka misaada huko Tel Aviv.
Kinyume na mahesabu potofu ya maafisa wa utawala wa Kizayuni, athari mbaya za sera za vita za Tel Aviv hazitawafikisha kwenye malengo yao maovu, na uungaji mkono wa watu kwa makundi ya Muqawama na mapambano utaongezeka zaidi.