Italia yaijia juu Israel kwa kushambulia kwa mabomu kanisa Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i128452-italia_yaijia_juu_israel_kwa_kushambulia_kwa_mabomu_kanisa_gaza
Waziri Mkuu wa Italia, Giorga Meloni jana Alkhamisi alikosoa vikali shambulio baya la Israel dhidi ya Kanisa la Kikatoliki katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2025-10-16T03:06:03+00:00 )
Jul 17, 2025 15:13 UTC
  • Italia yaijia juu Israel kwa kushambulia kwa mabomu kanisa Gaza

Waziri Mkuu wa Italia, Giorga Meloni jana Alkhamisi alikosoa vikali shambulio baya la Israel dhidi ya Kanisa la Kikatoliki katika Ukanda wa Gaza.

Wanawake wawili waliuawa katika shambulio hilo, kulingana na ripoti za vyombo vya habari. "Uvamizi wa Israel huko Gaza pia ulilenga Kanisa la Holy Family. Mashambulizi dhidi ya raia ambayo Israel imekuwa ikifanya kwa miezi kadhaa hayakubaliki," Meloni ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X.

Hakuna hatua ya kijeshi inayoweza kuhalalisha hatua za Israel, ameongeza Waziri Mkuu wa Italia katika ujumbe wake huo wa kulaani hujuma za kinyama za Israel dhidi ya Gaza.

Kadhalika Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Antonio Tajani pia amelaani shambulio hilo na kulielezea kama "tendo zito dhidi ya mahali pa ibada ya Kikristo," akiongeza kuwa ni "wakati umefika wa kusimamisha (mashambulizi) na kutafuta amani."

"Mashambulizi ya jeshi la Israel dhidi ya raia huko Gaza hayakubaliki tena," Tajani ameandika kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa X.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Italia ameeleza bayana kuwa, kunapaswa kuchukuliwa hatua za kuzuia kuwa mbaya zaidi hali hatarishi na tete Gaza na katika eneo la Asia Magharibi. 

Mara kwa mara, wananchi wa Italia na Wapalestina wanaoishi katika nchi hiyo ya Ulaya wamekuwa wakiandamana na kulaani vikali jinai za utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Gaza huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.