Nini lengo la Umoja wa Ulaya katika kuzidisha vikwazo dhidi ya Iran?
Umoja wa Ulaya, ukifuata nyayo za Marekani, umeendeleza siasa za kuzidisha mashinikizo dhidi ya Iran katika nyanja mbalimbali katika muhula wa pili wa uongozi wa Donald Trump kwa shabaha ya kuilazimisha Tehran isalimu amri mbele ya matakwa ya kupindukia mipaka ya nchi za Magharibi.
Katika hatua ya hivi karibuni zaidi, Umoja wa Ulaya, Jumanne Julai 15, uliweka vikwazo kwa watu wanane na chombo kimoja kuhusu masuala ya haki za binadamu yanayohusiana na Iran. EU imedai kuwa watu hao wanahusika na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu nje ya nchi kwa niaba ya Iran. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mali za watu binafsi na taasisi zilizowekewa vikwazo zimezuiliwa, na makampuni na raia wa Umoja wa Ulaya wamepigwa marufuku kufanya miamala ya kifedha na watu na taasisi hizo. Pia, watu waliowekewa vikwazo hivyo wamepigwa marufuku kuingia au kupita katika nchi za Ulaya.

Katika kujibu vikwazo hivyo vipya vya Umoja wa Ulaya, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imezitaja tuhuma za eti kukiuka haki za binadamu za Umoja wa Ulaya kuwa ni jaribio la kupindisha maoni ya umma kutoka kwenye suala muhimu zaidi la kipindi hiki, yaani mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel kwa msaada wa nchi za Maghjaribi dhidi ya watu wa Palestina, na uchochezi wa Israel katika eneo la Magharibi mwa Asia.
Hadi sasa Umoja wa Ulaya haujachukua hatua yoyote madhubuti ya kukabiliana na mauaji ya kimbari yanayofanywa na Isarel huko Gaza. Kwa mfano tu, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya walikutana mjini Brussels siku ya Jumanne kujadili suala la kusimamisha makubaliano ya ushirikiano na Israel na kuuwekea vikwazo utawala huo ghasibu kutokana na uhalifu wa kivita unaofanyika Gaza, lakini hakuna hata moja kati ya mapendekezwa yaliyowasilishwa, lililopasishwa katika kikao hicho ikiwa ni pamoja na kusimamisha makubaliano ya biashara, vikwazo vya silaha au vikwazo vya visa. Suala hili linaashiria kuwa, ukosoaji wa maneno tu wa Umoja wa Ulaya dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel ni propaganda tupu na kwamba umoja huo unaunga mkono kikamilifu utawala wa Kizayuni katika ukandamizaji na mauaji ya kimbari ya Wapalestina.
Kuhusiana na suala hilo, Amnesty International imelaani uamuzi wa Umoja wa Ulaya wa kutosimamisha makubaliano ya biashara ya upendeleo na utawala wa Kizayuni na kuutaja kuwa ni "ukatili na usaliti usiokubalika" kwa sheria za kimataifa na haki za Wapalestina.
Wakati huo huo, mwelekeo wa Umoja wa Ulaya na Troika ya EU (Ujerumani, Ufaransa na Uingereza) kuhusu Iran unatokana na ushirikiano kamili wa umoja huo na Marekani katika kuzidisha mashinikizo dhidi ya Iran kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine, tishio la kutekeleza mfumo eti wa kuilazimisha Iran isalimu amri kwa matakwa ya kupindukia mipaka ya nchi za Magharibi, ambayo sasa yanajumuisha sio tu kusimamisha urutubishaji wa madini ya uranium, lakini pia kubana uwezo wa makombora wa Iran na siasa za Jamhuri ya Kiislamu za kuunga mkono harakati za Muqawama na mapambano katika eneo la Magharibi mwa Asia.
Katika msimamo wa hivi karibuni wa Troika ya Ulaya kuhusu suala hili, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noël Barrow alitangaza mbele ya mkutano wa Baraza la Mahusiano ya Kigeni la Umoja wa Ulaya siku ya Jumanne kwamba Troika ya Ulaya itaanzisha utaratibu wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran maarufu kama snapback ifikapo mwisho wa Agosti 2025 ikiwa hakuna maendeleo yanayoonekana katika mazungumzo ya nyuklia.
Kuanzisha utaratibu huo kunaweza kurejesha moja kwa moja vikwazo vyote vya awali vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran. Vikwazo hivyo vya kimataifa dhidi ya viwanda vya silaha, fedha na benki za Iran, na sekta ya nyuklia viliondolewa miaka 10 iliyopita. Tishio hilo jipya la Umoja wa Ulaya limekuja katika hali ambayo, baada ya Marekani kujitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mwezi Mei 2018, nchi za Ulaya, kinyume na majukumu yao, hazikuchukua hatua yoyote ya kupunguza athari za vikwazo vya Washington, na badala yake ziliitaka Iran itekeleze majukumu yake ndani ya makubaliano ya JCPOA.

Baada ya kuanza mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani, nchi za Ulaya, ambazo zilijiona zimetengwa na kudhalilishwa na Rais wa Marekani Donald Trump, sasa zimependekeza wazo la kuanzishwa utaratibu wa snapback ili kuwa na nafasi tena katika suala la nyuklia la Iran. Hii ni licha ya kwamba suala la kuanzishwa tena mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani bado limegubikwa na sintofahamu.
Awali, maafisa wa Iran walikuwa wameonya kwamba, hatua yoyote ya upande mmoja ya Troika ya Ulaya itakabiliwa na jibu linalofaa kutoka kwa Tehran, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kujiondoa kwenye mtataba wa NPT.