Jeshi la IRGC Laangamiza magaidi sita katika operesheni kusini mashariki mwa Iran
Kikosi cha Nchi Kavu cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu cha Iran (IRGC) kimewapa pigo kali magaidi wanaoungwa mkono na maadui, katika operesheni kubwa ya kupambana na ugaidi inayofanyika katika jimbo la kusini mashariki la Sistan na Baluchestan, karibu na mpaka wa Pakistan.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kituo cha Quds cha Jeshi la IRGC iliyotolewa Jumanne jioni, maficho ya wanachama kadhaa wa makundi ya kigaidi yaligunduliwa katika mji wa pwani wa Chabahar, kutokana na uelewa wa wananchi wa eneo hilo. Haya yamejiri wakati mazoezi makubwa ya kijeshi yanayojulikana kama "Mashujaa wa Usalama" yakiendelea.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa jeshi hilo lilifanikiwa kuwaangamiza magaidi sita kwa operesheni ya haraka na ya kisasa. Aidha magaidi hao waliouawa walipatikana wakiwa na idadi kubwa ya silaha.
Jeshi la IRGC lilibainisha kuwa magaidi waliouawa walikuwa na mipango ya kutekeleza mfululizo wa mashambulizi ya kigaidi katika maeneo yenye misongamano ya watu.
Jimbo la Sistan na Baluchestan, linalopakana na Pakistan, likikumbwa mara kwa mara na mashambulizi ya kigaidi dhidi ya raia na maafisa wa usalama kwa miaka kadhaa sasa.
Makundi ya kigaidi yanayolenga maslahi ya Iran hasa katika maeneo ya kusini mashariki na kusini magharibi mwa nchi yanaaminika kuwa na uhusiano wa karibu na mashirika ya kijasusi ya mataifa ya kigeni.
Mnamo tarehe 26 Oktoba mwaka jana, maafisa 10 wa vikosi vya usalama vya Iran waliuawa katika shambulizi la kigaidi lililotokea katika wilaya ya Gohar Kuh, Kaunti ya Taftan, jimboni humo.
Kundi la kigaidi linalojiita 'Jaish al-Adl' lilidai kuhusika na shambulizi hilo, ambalo lilikuwa miongoni mwa mashambulizi mabaya zaidi kutokea katika eneo hilo katika miezi ya karibuni.
Kundi hilo limewahi kufanya mashambulizi mengi ya kigaidi nchini Iran, hasa katika jimbo la Sistan na Baluchestan. Mbinu zake ni pamoja na utekaji wa walinzi wa mipaka, kushambulia raia, na vituo vya polisi kwa nia ya kuchochea machafuko na hali ya taharuki.