Trump ashadidisha vita vya kibiashara dhidi ya Mexico, EU
https://parstoday.ir/sw/news/world-i128266-trump_ashadidisha_vita_vya_kibiashara_dhidi_ya_mexico_eu
Rais Donald Trump wa Marekani ametishia kuziwekea bidhaa zinazoingia nchini humo kutoka Mexico na Umoja wa Ulaya ushuru wa asilimia 30 kuanzia Agosti Mosi.
(last modified 2025-10-20T07:03:11+00:00 )
Jul 13, 2025 06:04 UTC
  • Trump ashadidisha vita vya kibiashara dhidi ya Mexico, EU

Rais Donald Trump wa Marekani ametishia kuziwekea bidhaa zinazoingia nchini humo kutoka Mexico na Umoja wa Ulaya ushuru wa asilimia 30 kuanzia Agosti Mosi.

Trump ametangaza ushuru huo mpya katika barua alizowatumia Rais wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen na Rais wa Mexico, Claudia Sheinbaum.

Haya yanajiri baada ya mazungumzo ya wiki kadhaa baina ya Marekani na washirika wake hao wakubwa wa kibiashara kugonga mwamba.

Mexico na Umoja wa Ulaya zimekosoa vikali ushuru huo mpya wa forodha wa Marekani, zikisisitiza kuwa ushuru huo sio wa kiadilifu na kwamba hautakuwa na matokeo mengine ghairi ya kushadidisha vita vya kibiashara duniani.

Vitendo vya Rais Donald Trump wa Marekani hususan kushadidisha vita vya kibiashara na dunia ambavyo vimesababisha machafuko katika mfumo wa uchumi na biashara wa kimataifa, vimeufanya Umoja wa Ulaya kutaka kupanua na kuimarisha uhusiano wake na nchi za Bahari ya Pasifiki (Trans-Pacific).

Ikumbukwe kuwa, Ikulu ya Rais wa Marekani ilitangaza hivi karibuni kwamba, bidhaa zinazoingizwa Marekani kutoka China sasa zitatozwa ushuru wa asilimia 145, na huenda ukapindukia asilimia 200.