Maafisa wa Syria na Israel wanatazamiwa kukutana Baku
Maafisa wa Syria na Israel wanatazamiwa kukutana mjini Baku ili kujadili "uwepo wa hivi karibuni wa jeshi la Israel nchini Syria.
Chanzo cha habari cha kidiplomasia mjini Damascus kililiambia shirika la habari la AFP jana Jumamosi kwamba, maafisa hao wa Syria na Israel wanatarajiwa kukutana mjini Baku pambizoni mwa ziara ya Abu Mohammed al-Jolani nchini Azerbaijan.
Chanzo hicho ambacho kiliomba kutotajwa jina, kiliongeza kuwa Jolani, mkuu wa Utawala wa Hay’at Tahrir al-Sham (HTS) unaoongoza nchini Syria, hatahudhuria mkutano huo binafsi.
Israel, muuzaji mkuu wa silaha kwa Azerbaijan yenye uwepo mkubwa katika taifa hilo la Caucasia, imefanya mamia ya mashambulizi ya anga nchini Syria tangu magenge ya wanamgambo wakiongozwa na Hay’at Tahrir al-Sham ya Jolani, kumpindua Rais Bashar al-Assad mwezi Desemba.
Israel pia imetuma wanajeshi katika eneo la kiraia linalosimamiwa na Umoja wa Mataifa, ambalo hapo awali lilitenganisha vikosi pinzani kwenye Miinuko ya Golan, kufuatia kuangushwa kwa serikali ya Assad.
Utawala mpya wa Syria umekuwa ukiashiria nia ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Tel Aviv. Pande hizo mbili zinaripotiwa kushiriki katika mazungumzo ya kufikia makubaliano ya kuanzisha uhusiano wa pande mbili ifikapo 2026.
Utawala wa Hay’at Tahrir al-Sham (HTS) unaoongoza nchini Syria, tawi la zamani la al-Qaeda, pamoja na wanamgambo wengine, walichukua udhibiti wa Damascus mnamo Disemba 8, 2024, na kumfurusha Rais Bashar al-Assad nchini humo.